Monday, August 23, 2010

JK: Mimba kwa wanafunzi ni kiherehere chao


NA MWANDISHI WETU

7th June 2010



Rais Jakaya Kikwete amesema matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe.



Aidha, Rais Kikwete amekiri kwamba matukio ya mauaji ya vikongwe pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), yanalidhalilisha taifa.



Rais Kikwete alitoa kauli hizo katika kijiji cha Kisesa wilayani Magu jana wakati akihutubia wananchi kwenye ufunguzi wa mashindano ya ngoma kwa kabila la Wasukuma; ngoma ambazo zinajulikana kama 'Bulabo'.



" Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule," alisema Rais Kikwete wakati akijibu risala ya Mkurugenzi wa Makumbusho ya Bujola, Fadha Frasince Sandhu, ambaye alisema ujumbe wa mashindano hayo mwaka huu ni vita dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.



Kwa mujibu wa Rais Kikwete, suala la zinaa kwa bianadamu, siyo la lazima hivyo binadamu anaweza kujizuia ama kujikinga kwa kutumia kondomu.



" Na kwa bahati mbaya shughuli ile (uzinzi) binadamu hana dharura nayo, hivyo unaweza kutumia kondomu kama unaona kwamba huwezi kutii amri ya sita ama huwezi kuwa mwaminifu katika ndoa yako," alisema kauli ambayo ilizua vicheko miongoni mwa watu waliohudhuria ufunguzi huo. Aliwashauri wananchi watakaoshiriki kwenye mashindano hayo wawe na tahadhari dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.



" ...katika mambo yanayolitia aibu taifa hasa kwa watani wangu Wasukuma, ni pamoja na mauaji ya albino na vikongwe eti tu kwa sababu wana macho mekundu. Ni mambo ya fedheha sana ingawa yanakwenda yanapungua lakini yanalidhalilisha taifa," alisema.



Aliwataka washiriki wa mashindano hayo walisaidie taifa katika kupiga vita mauaji ya aina hiyo.



Rais Kikwete alifuatana na wabunge kadhaa akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (CCM) pamoja na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM).



Aidha, Rais Kikwete amepewa jina la Mungubabu, ikiwa na maana busara na uwezo wa kuongoza nchi kama Mungu.



Mashindano ya 'bulabo' yalianza mwaka 1954 kupitia Kanisa Katoliki Bujola, lengo likiwa ni kuweka burudani mara baada ya mavuno.



CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment