Monday, August 16, 2010

Kuenguliwa kwa Mwakalebela kwasababisha vurugu Iringa


Monday, 16 August 2010

Mwananchi



BAADA ya halmashauri kuu ya CCM kumuengua Fredrick Mwakalebela kugombea ubunge wa Iringa Mjini, kundi la wanachama wa chama hicho tawala wameahidi kurudisha kadi kwenye ofisi za matawi yao kuanzia leo kuonyesha kutoridhishwa na mchakato huo.



Halmashauri kuu, ambayo ilimaliza kikao chake mjini Dodoma Jumamosi, ilimuengua katibu huyo mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka (TFF) kwa sababu zilizoelezwa kuwa za kimaadili licha ya Mwakalebela kushinda kwa kura 3, 897 dhidi ya 2,989 za mpinzani wake, Monica Mbega, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na ambaye anatetea kiti chake.



Mwakalebela ni kati ya wagombea watatu walioshinda kwenye kura za maoni na wakaenguliwa na Nec na pia ni kati ya wagombea watatu waliofikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai ya kutoa rushwa licha ya wagombea wengi wa CCM kuhojiwa na wengine kukamatwa na taasisi hiyo kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa.



Mwananchi ilitembelea baadhi ya matawi ya chama hicho mjini hapa na kushuhudia makundi ya wanachama wakijipanga na kuendelea kuwashawishi wenzao jinsi kuzirudisha kadi za CCM katika ofisi za matawi yao.



Wanachama hao, ambao walikuwa wakitafakari uamuzi huo wa halmashauri kuu, walikuwa wakishawishiana kuiunga mkono Chadema ambayo imemsimamisha Mchungaji Peter Msigwa kuwania jimbo hilo.



Wanachama hao ni wa matawi ya Mwangata, Ruaha, Kichangani, Mtwivila, Kihesa, Wilolesi, Soko Kuu la Mjini Iringa, Mshindo na Igumbilo ambako wanachama walionekana kuguswa na uamuzi wa kumuengua Mwakalebela.



Baadhi ya wanachama hao walisema uamuzi wa halmashauri kuu ni wa kumtoa kafara Mwakalebela ambaye Takukuru ilimuhoji kwa tuhuma za kutoa rushwa kwenye vijiji viwili.



“Tumemchoka Monica Mbega; tulichotaka ni kubadilisha uongozi... hizi taarifa za Takukuru zinadai kwamba kwa kupitia mke wake ambaye naye hakukamatwa akifanya hivyo," alisema mmoja wa wanachama hao aliyejitambulisha kwa jina la David Butinini wa tawi la Mtwivila "Mwakalebela alitoa ushwa ya Sh 100,000 kwa wanachama 22 wa kijiji cha Mgongo, habari hizo zinaaminikaje wakati bado kesi haijaisha? Waturudisheie.”



Naye July Sawani wa tawi la Kichangani, alisema wakati Mwakalebela akienguliwa kwa madai hayo ya rushwa, inashangaza kuona Nec hiyo hiyo imeyapitisha majina ya Basil Mramba na Andrew Chenge ambao wana tuhuma kubwa tena nzito kuliko ya Mwakalebela.



Alli Mduba wa tawi la Kihesa alisema uamuzi wa CCM wa kuwataka wanachama wote washiriki katika kura hizo umekiwezesha chama hicho kujua wagombea wanaokubalika katika mbio hizo za uongozi, hata hivyo akasema majibu ya uamuzi uliofanywa na halmashauri kuu dhidi ya Mwakalebela yatayapata Oktoba 31 ambayo ni siku ya uchaguzi mkuu.



Mohamed Kassim wa Wilolesi alisema leo wanachama watarudisha kadi zao za CCM kwenye ofisi ya tawi katika tukio ambalo pia watalitumia kumtangaza rasmi mgombea watakayemuunga mkono.



Naye Edgar Sanga wa Igumbilo alisema wanachama watamaliza jazba zao za mgombea wao kuenguliwa kwa kumpigia kampeni na kura mgombea wa Chadema.



“Mwakalebela ndiye aliyekuwa chaguo letu vijana na wananchi wote wa jimbo la Iringa Mjini bila kujali rangi, itikadi, dini na makabila yao , tumesikitishwa na uamuzi wa NEC,” alisema mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Anna Michael wa tawi la Miyomboni.



Wakati wanachama hao wa CCM wakijiandaa kurejesha kadi, Chadema wanasherehekea wakidai kwamba sasa ni rahisi kulichukua jimbo kwa madai kuwa mgombea aliyekuwa tishio ni Mwakalebela ambaye alikuwa na kundi kubwa la vijana.

No comments:

Post a Comment