Monday, August 23, 2010

Urais ni kazi tukufu na Ikulu ni mahali patakatifu


Urais ni kazi ya watu, kazi yoyote ya kuhudumia watu ni kazi ya kumtumikia Mungu!



Hii ni kazi tukufu na Ikulu ni mahali patukufu hapataki kuwa sehemu ya mzaha, uongo, ulaghai na unyang'anyi ambao tunauona leo ukisimamiwa na watawala wetu tuliowaamini na kuwapa idhini wakae Ikulu.

Kama Ikulu ingelisema wale wote waliohusika na wizi wa EPA, Deep Green Finance, Mwananchi Gold, IPTL, RITES, n.k wawajibishwe kwa mjibu wa SHERIA bila woga wala upendeleo na kwa dhati, idara husika zingelihakikisha wahusika wa Kagoda wanashughulikiwa, wahusika wote waliolitumia jeshi letu tukufu kwa manufaa yao ya kifedhuri wangewajibishwa na wala hakuna mwanajeshi ambaye angelileta fujo kupinga kwa sababu hili ni jeshi la wananchi kwa ajili ya wananchi. Wale wote waliohusika na mikataba mibovu ilitufikisha hapa tulipo wangelikuwa viranja katika magereza yetu na si kwenye majukwaa ya kuomba kuwatumikia watu..... wengine wakiwawekea watanzania safi vipingamizi ili wasiweze kupambana na hasira za wananchi katika masanduku ya kura... hawa wote wangelikuwa wanawajibika kadri ya matendo yao na Tanzania yetu ingelikuwa na matumaini makubwa na amani kama waasisi wa taifa hili walivyotaka Tanzania iwe.



Wale wote ambao wanatufanyia mzaha katika zoezi muhimu la uchaguzi wasingefanya vile wanavyofanya, wasingelithubutu!



Tunataka mtu atakayeomba kwenda Ikulu afanye hivyo kwa manufaa yetu sote na si kulinda maslahi ya wachache, vinginevyo malaika wa watanzania maskini wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma za msingi (kwa sababu haki yao imetwaliwa na hao wachache wanaolindwa na watawala wetu) itawaandama na kuwafanya waweweseke na kuaibika mbele ya dunia.



Mungu Ibariki Tanzania na Nguvu zako kuu zishuke kwa wale wote wanaoifanyia mzaha kazi yako

No comments:

Post a Comment