Monday, August 23, 2010

Vituko vya kampeni vyaanza


• Mkutano wa Mrema TLP wavurugwa





na Mwandishi wetu









VITUKO vya kampeni za uchaguzi mkuu vimeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro kuelezea kukerwa na mwenendo wa viongozi wake walioamua kumpigia debe mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) , Philemon Ndesamburo, katika jimbo la Moshi Mjini.

Hatua ya viongozi wa CCM kumpigia kampeni inaelezwa na wanachama wake kuwa ni kutokubaliana na maamuzi yaliyofanywa Halmashauri Kuu ya (CCM) kumwengua mshindi wa kura za maoni Athuman Ramole.



Chama hicho kimesema kiko tayari kuwafukuza wanachama na viongozi wote watakaobainika kutokana na utovu wa nidhamu kwa kushindwa kukubaliana na maamuzi ya NEC.



Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Steven Kazidi, aliyasema hayo juzi wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho , Justine Salakana, kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake kwenye viwanja vya Manyema.



Alisema kuna wanachama ambao ni viongozi ndani ya CCM, wamekuwa wakizunguka usiku wakitumia usafiri wa pikipiki wakidai wameonewa kwa kuwa mgombea waliyemtaka Buni hakuteuliwa licha ya kushinda, hivyo kuwashawishi wana CCM wampigie kura mgombea wa CHADEMA.



MAREALE



Naye Kamanda wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Manispaa Moshi Aggrey Mareale, alisema itakuwa vigumu katika kampeni zinazoendelea kusimama jukwaani na kuacha kumsifia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Philemoni Ndesamburo.



Marealle aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo uliofanywa katika viwanja vya Manyema vilivyoko mjini hapa.



Alisema hata kama mbunge huyo aliweza kujenga madarasa 10 ya shule ndiyo jitihada zake, lakini huenda ameshindwa kutosheleza mahitaji ambayo yalikuwa yanahitajika katika jimbo zima.



MOSHI



Habari zaidi kutoka Moshi, zinasema wakati kampeni zikiwa zinaendelea katika maeneo mbalimbali, juzi katika mkutano wa wa mgombea ubunge wa jimbo la Vunjo, Agustine Mrema, uliingia dosari baada ya Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kahe kusababisha vurugu zilizosabisha mkutano wake kusimama kwa muda.



Vurugu hizo, ambazo zilidumu kwa takriban dakika 15 na kupelekea wananchi waliohudhuria mkuatano huo kupoteza usikivu, wakati Mrema alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kahe na hivyo kulazimika kutoa fursa kwa wasimamizi wa mkutano kufanya jitihada za makusudi kutuliza vurugu hizo.



Akizungumza baada ya kutokea kwa vurugu hizo, Anael Mmamyi ambaye anawania nafasi ya udiwani kupitia TLP kata ya kahe, alisema kuwa ni vyema kama vyama vya siasa vinafanya mikutano yake na kuhudhuriwa na upinzani; ni vyema wakawa na nidhamu ili kuepuka vurugu inayoweza kupelekea kuwepo kwa uvunjifu wa amani.



Katika mkutano huo, Mrema alisisitiza kuwa lengo la kujitokeza kuwania kiti cha ubunge kwenye jimbo hilo ni kuhakikisha aliahidi kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kufufua mifeji ya zamani kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuweka kipaumbele katika sula la elimu.



KAHAMA



Pingamizi la mgombea ubunge katika jimbo la Msalala kwa tiketi ya CCM, Ezekiel Maige, alilomwekea mgombea wa CHADEMA, Edward Mlolwa, limegonga mwamba baada ya Kamati ya Maadili ya Jimbo la Kahama na Msalala kumthibitisha ni mgombea halali.



Kwa mujibu wa barua ya Agosti 21 aliyoandikiwa Maige na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kahama na Msalala, Eliza Bwana, na nakala kupatiwa mgombea wa CHADEMA ambayo Tanzania Daima imepata nakala yake, ilieleza baada ya kupitia maelezo ya pingamizi, Kamati ya Maadili imejiridhisha kuwa Mlolwa ni mgombea halali wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Msalala kwa tiketi ya CHADEMA.



Maige ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na ambaye hakupata mpinzani katika mchakato wa kura za maoni za chama chake, aliwakilisha pingamizi lenye vipengele 12 dhidi ya mgombea huyo.



Miongoni mwa mapingamizi hayo ambayo kamati hiyo imeyapitia na kuyathibitisha kuwa hayana dosari ya kumzuia Mlolwa kuwania ubunge ni juu ya kutodhaminiwa na chama chake, uanachama wake wa CHADEMA, kudhaminiwa na wapiga kura, kutowasilisha tamko la kisheria na kutowasilisha mchanganuo wa gharama za uchaguzi.



Kwa mujibu wa barua ya msimamizi wa uchaguzi, tume ilimfafanulia Maige kuwa Mlolwa amedhaminiwa na chama chake cha siasa kwa kujaza fomu ya uteuzi iliyosainiwa na katibu wa chama chake.



Ni mwanachama halali wa chama chenye usajili ambaye amedhaminiwa na wapiga kura walioandikishwa katika madaftari ya wapiga kura wa jimbo, pia aliwasilisha tamko la kisheria lililosainiwa na hakimu Agosti 19, mwaka huu.



SINGIDA



Habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni, zinasema mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Singida, Mohamed Dewji, amepita bila kupingwa.



Taarifa iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Yohana Lucas Maki, ilisema pingamizi lililokuwa limewekwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Josephat Isango Hadu, limetupwa.



Katika uwamuzi huo, msimamizi huyo alisema Dewji hajatenda vitendo vya rushwa kama Sheria ya Gharama ya Uchaguzi inavyoelekeza.

No comments:

Post a Comment