Thursday, August 19, 2010

Wapinzani sasa waja na 'Mbeya kwanza vyama baadaye'




Felix Mwakyembe, Mbeya Agosti 18, 2010





Kutosimamisha mgombea Rungwe Mashariki na Kyela



Sugu kupambana na mwalimu wake





Maamuzi ya NEC CCM yawakosha Mbeya





WAKATI uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukipitisha majina ya wote waliongoza kwenye kura za maoni mkoani Mbeya, vyama saba vya upinzani mkoani humo vinashirikiana kuhakikisha vinaiengua CCM.

Vyama hivyo vimekuja na kauli mbiu ya “Mbeya kwanza vyama baadaye,” ikiwa na maana kwamba la msingi kwao ni maendeleo ya mkoa huo na si kitu kingine, kwamba vyama ni utaratibu tu wa kisheria kwa wenye nia ya uongozi kupitia, hivyo kutoa nafasi hata kwa Chama cha Mapinduzi, ambacho kwa miongo kadhaa sasa kimehodhi siasa na uongozi wa nchi, kushiriki katika ushirika huo.



Mwenyekiti wa ushirika huo, Godfrey Davis, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya wa chama cha APPT, analitaja lengo lao kuwa ni kutekeleza kilio cha siku nyingi cha umma kuvitaka vyama vya Upinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja badala ya kushindana wenyewe kwa wenyewe kwenye kusimamisha wagombea hata pale ambapo chama kina uhakika hakina nguvu.



Hata hivyo, katika ushirika huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakimo, chenyewe tayari kimempitisha mwanamuziki Joseph Mbilinyi kuwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini ambako atapambana na mwalimu wake, Benson Mpesya.



Mkakati wa vyama hivyo katika ushirika wao ni kuangalia mgombea anayekubalika miongoni mwa wagombea wao wote na ambaye ndiye atakuwa mwakilishi wa vyama hivyo kwenye udiwani au ubunge lakini akipitia kwenye moja ya vyama hivyo, lakini huku wakibainisha kutokuweka wagombea ubunge kwenye majimbo ya Kyela na Rungwe Mashariki.



“Mwaihojo akikubali atachangiwa pesa za kuchukulia fomu, tutatumia nguvu ya umma, kuhusu atapitia chama kipi atachagua mwenyewe, lakini kwa Rungwe Mashariki na Kyela hatuoni sababu ya kuweka mgombea, tumeridhika na utendaji wa wabunge waliopita, kipaumbele chetu ni maendeleo ya Mbeya kwanza na si vyama,” anasema Yasin Mrotwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Mkoa wa Mbeya.



Kimsingi, jicho la vyama hivi linaliangalia Jimbo la Mbeya Mjini zaidi ambalo wamepania kulichukuwa wakisema ndiyo taswira ya mkoa, kwamba sasa linatia aibu kutokana na kuporomoka katika kila nyanja ikiwamo elimu, ni katika jimbo hilo ambapo vyama hivyo vinaweka wagombea kwenye kila kata na nafasi ya ubunge.



Vyama vilivyomo kwenye ushirika huo ni pamoja na APPT-Maendeleo, NCCR-Mageuzi, TADEA, SAU, TLP, CUF na UDP, ambavyo kwa pamoja vilikubaliana kumuomba mwanachama wa CCM, Prince Mwaihojo awe mgombea wao.



Pamoja na ushirika huo, Mwaihojo anakabiliwa na kibarua kigumu katika Jimbo hilo la Mbeya Mjini kutokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) kurudisha jina la mbunge aliyepita Mpesya, ambaye nguvu zake za kisiasa zimezidi kuimarika kwa kuungwa mkono na wabunge wengine watarajiwa kama Profesa Mark Mwandosya.



Wachambuzi wa masuala ya siasa za Mbeya wanabainisha kuwa Mpesya alicheza karata yake vizuri kwenye chaguzi za CCM pale aliposimamia kampeni iliyobatizwa jina la “Linda heshima ya Mbeya,” ikiwa na maana ya kuhakikisha Profesa Mwandosya anarudi kwenye NEC kupitia mkoa huo, hatua hiyo ilimuongezea watu wa kumunga mkono.



Ni wazi mgombea aliyepitishwa na CHADEMA mwanamuziki Mbilinyi hatokuwa tayari kuondoa jina lake kumpisha Mwaihojo, hivyo vyama vya wapinzani watagawana kura zisizoegemea kundi lolote wakati mwenzao Mpesya atakuwa na mtaji wake wa kura na kuchota nyingine kwenye kapu la wasio na upande.



Hadi Jumatatu ni vyama vya CCM na CHADEMA tu vilivyokuwa vimetangaza majina ya wagombea wao katika majimbo yote ya Mbeya, na ni vyama hivyo ambavyo vinatarajiwa zaidi kukabana makoo, huku matumaini makubwa kwa CHADEMA yakiwa kwenye Jimbo la Mbeya Vijijini ambako mbunge aliyemaliza muda, Luckson Mwajale (Mbeya Vijijini) atakabiliana na mpizani wake mkuu Sambwee Shitambala Mwalyego.



Mwanjale aliingia bungeni kupitia uchaguzi mdogo uliotishwa kwenye jimbo hilo baada ya kifo cha mbunge wake wa awali, Richard Nyaulawa, uchaguzi ambao ulilalamikiwa na wadau wengi wa siasa hapa nchini kutokana na hatua ya kuenguliwa kwa Shitambala, mgombea aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda, ni imani ya wananchi kuwa Oktoba mwaka huu hakutakuwa na ujanja ujanja tena, watapambana.



Wananchi hawatarajii upinzani wowote kwenye Jimbo la Kyela ambako mbunge aliyemaliza muda wake Dk. Harrison Mwakyembe amepitishwa tena kuwania nafasi hiyo wakati CHADEMA wamempitisha Katibu wa chama hicho mkoani Mbeya, Edo Makatta.



Hali ni hivyo hivyo kwa Jimbo la Rungwe Mashariki ambako Profesa Mwandosya ameteuliwa tena kugombea nafasi hiyo huku CHADEMA wakimteua Gwakisa Mwakasendo. Victor Mwambalaswa katika Jimbo la Lupa wilayani Chunya naye amepitishwa tena na chama chake cha CCM na anatarajia kupambana na George Mtasha aliyepitishwa na CHADEMA.



Mpambano wa CCM na CHADEMA mkoani Mbeya unatarajiwa pia kuonekana katika Jimbo la Mbarali ambako CCM imepitisha jina la Dickson Modestus Kilufi wakati CHADEMA imempitisha Jidawaya Kazamoyo, Jimbo la Songwe wilayani Chunya CCM imepitisha jina la Philipo Augustino Mulugo wakati Chaddema imepitisha jina la Hamad Mwalyonde.



Majimbo mengine ni pamoja na Rungwe Magharibi ambako CCM imempitisha Profesa David Mwakyusa huku CHADEMA ikimpitisha Gwakisa Mwakasendo, Jimbo la Ileje CCM imempitisha Aliko Kibona na CHADEMA ikiwa imempitisha Henry Kayuni, Jimbo la Mbozi Mashariki CCM imempitisha Godfrey Zambi wakati CHADEMA imempitisha Mpale Mwampamba na Dk. Luka Siame amepitishwa katika Jimbo la Mbozi Magharibi ambako nao CHADEMA wamempitisha David Silinde.



Hatua ya NEC CCM kurudisha majina ya wanachama wake walioshinda, hususani wabunge waliomaliza muda wao na kuongoza kura za maoni imepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa vyama hivyo viwili mkoani humo lakini kwa ujumla wananchi wengi wameonyesha kufurahia kutokana na imani yao kwa wabunge hao huku kwa wanachama wa CHADEMA wakikosa raha kwa sababu walitarajia kuvuna vigogo hao iwapo wangetemwa.



Mitazamo yote ya wananchi hao mkoani Mbeya ilijengeka kutokana na taarifa zilizovuja kutoka katika Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mbeya kwamba wabunge hao walipewa alama E, kwamba hawafai kuwa viongozi, taarifa zilizopeleka faraja CHADEMA kwani kwao ulikuwa mtaji mnono lakini wakati huo huo zikapeleka simanzi kwa wanachama wa CCM kwa kuwa waliamini hatua hiyo ingeyatoa kiulaini majimbo takribani yote kwa CHADEMA kwa vigogo hao kutimkia huko.



Pamoja na kuwakosa vigogo hao, bado CHADEMA kinaendelea kuvuna kwenye kata ambako, mathalani katika Kata ya Ipinda pakee, kinatarajia kuvuna zaidi ya wanachama 1,500 kutoka CCM waliokasirishwa na hatua ya Kamati ya Siasa mkoani humo kumuengua mwanachama aliyeongoza kwenye kura za maoni, Spaita Mwampuga na badala yake kupitisha jina la tabibu, Hunter Mwakifuna.



Wananchi hao wanaamini kuwa Mwakifuna amepitishwa kwa shinikizo la Mkuu wa Mkoa huo, John Mwakipesile ambaye hata hivyo aliikwiahakukanusha kuhusika katika sakata hilo, na zaidi ya hapo wanaamini kuwa pamoja na kupitishwa amekiuka sheria ya uchaguzi serikali za mitaa kwa kuwa ni mtumishi wa Halmashauri ya Kyela ilimo kata ya Ipinda.



“Ipinda yote ipo nyuma ya Spaita, wasipotuletea tunamchagua diwani na Rais wa CHADEMA. Mwakyembe tumemaliza kazi, huyo ndiye mbunge wetu,” anasema Edward Mwakanosya wa Ipinda, na kauli yake hiyo inapokelewa na Mzee Hebron Mwalwisi (85) anayeongeza:



“Watu wanaiba kura, watu tupo hapa, waandishi mpo hapa mmeshuhudia lakini mko kimya, inauma sana.”



Pamoja na Ipinda, vile vile CHADEMA kinatarajia kuvuna kutoka Kata ya Makwale wilayani humo ambako Huruga Kalomba aliyeongoza kwa kura 299 ameenguliwa na nafasi hiyo kupewa Aliko Kasyupa anayedaiwa kupata kura 284.



Pamoja na migogoro hiyo inayotokana na kura za maoni katika vyama hivyo viwili, mchuano unatarajiwa zaidi kwenye nafasi ya udiwani ambako safari hii vijana wengi wamejitokeza kuwanania nafasi hizo kwa lengo la kutengeneza Halmashauri za Jiji na Wilaya zenye nguvu tofauti na ilivyo hivi sasa.



Lililo wazi ni kwamba nafasi ya upinzani kupata ushindi katika nafasi za ubunge na madiwani mkoani humo, hadi sasa unategemea zaidi msimamo wa vyama hivyo, vitapata ushindi pale tu vitakapokubali kuachana na ubinafsi wa kuwachukulia wananchi wa mkoa huo kiurahisi rahisi kama ilivyotokea katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005.



Siasa za Mkoa wa Mbeya zinategemea sana utamaduni wa wananchi wa mkoa huo ambao ni wakulima, wenye kumthamini mtu kutokana na utendaji wake, tabia yake na misimamo yake, kama kuna jambo wanalolichukia zaidi basi ni ile dharau ya kuwaamulia mambo yao, kwa lugha nyingine ni ile tabia ya wale waishio nje ya mkoa huo kuwapelekea watu ili wawe wawakilishi wao wakati hawajawahi kuishi nao, bila kujali kama ni Mnyakyusa, Msafwa, Mnyiha, Mbungu, Msangu au Mndali.

No comments:

Post a Comment