Monday, October 18, 2010

KIKWETE ANYIMWA USINGIZI

Dk. Slaa amnyima Kikwete usingizi

Mwandishi Wetu
Oktoba 13, 2010

Upepo wabadilika Rukwa, Katavi, Arusha na Mwanza

MGOMBEA urais kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete amebadili mwelekeo wa kampeni zake kwa kuanza kumshambulia mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, ambaye anaonekana kuanza kupanda chati muda mfupi tu kabla ya Uchaguzi Mkuu, Raia Mwema limebaini.
Mabadiliko hayo ya mwelekeo katika kampeni za Kikwete yanadhihirishwa katika matukio na kauli za hivi karibuni za ama yeye mwenyewe au za vyombo vya dola, yote yakionyesha kwamba sasa Dk. Slaa ni tishio la dhahiri dhidi ya CCM.
Katika mikutano yake ya hivi karibuni, Kikwete amebadili staili ya kampeni zake kwa kuanza kukosoa moja kwa moja hoja za Dk. Slaa ikiwamo kutoa elimu bure na kununua meli katika maziwa yote makuu nchini.
Katika kuelezea kuhusu suala la utoaji huduma za jamii bure, Kikwete sasa anadai kwamba hilo lilishindikana wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kinyume cha kauli za wapinzani kwamba viongozi na raia wengi wa sasa walisoma bure wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Tanzania.
Akiwa mkoani Ruvuma wiki hii, Rais Kikwete alisema ya kuwa ni udaganyifu mkubwa kwa chama chochote cha siasa kuahidi kuwa kinaweza kutoa huduma za jamii bure kwa wananchi na kwamba sera za kutoa huduma za jamii bure zilipata kujaribiwa kwa muda mrefu nchini chini ya uongozi wa Baba wa Taifa lakini zikashindikana.
Mbali ya Kikwete kukebehi ahadi na kauli za Dk. Slaa, ameanza kutoa madai kwamba wagombea wa Upinzani hawafai kuongoza nchi kwa kuwa wamekuwa wakitoa kauli za uchochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani.
“Huko nyuma chini ya Mzee wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere tulikwishakujaribu haya ya bure, lakini ikashindikana. Na sera hizo za bure tulizibadili chini ya uongozi wake mwenyewe Mzee Nyerere, chini ya uenyekiti wake, alisema Kikwete, mgombea anayetaka ridhaa ya kutetea kiti anachoshikilia sasa cha Urais wa Jamhuri.
“Tuliishia hakuna kitu chochote – maduka yalibakia tupu, hospitali dawa zilikuwa hakuna kabisa. Tunayakumbuka sana haya,” alisema Kikwete akiwahutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtyangibole, mkoani Ruvuma na kuongeza:
“Hakuna jipya katika sera hizi za bure. Tukizijaribu tena ni dhahiri na wazi kabisa kuwa katika miezi michache sana maduka yatakuwa hayana bidhaa, hospitali zitakuwa hazina dawa na huduma za jamii zitadorora sana katika kipindi kifupi.”
Kuhusu madai yake ya kwamba CHADEMA wanatishia umwagaji damu, Rais Kikwete alisema: “Hawa ni watu ambao siasa zimewashinda. Hawana jipya. Wapuuzeni. Wanataka nyie mtoane damu na wao wapande ndege kukimbilia Ulaya.”
Kuhusu ahadi nyingine ambayo imekuwa inatolewa na Dk. Slaa kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania atawapatia wananchi treni ya kasi ya kusafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza kwa kiasi cha saa tatu tu, Kikwete alisema:
“Saa tatu tu kufika Mwanza kwa treni? Hata ndege ya Rais yenye kasi sana inatumia saa mbili kufika Mwanza kutoka Dar es Salaam, sasa treni itachukuaje saa tatu tu?
“Ukimwona mtu mzima anawadanganya watu wazima wenzake wakati wote basi kuna mambo mawili. Moja ni kwamba ama mtu huyo ana matatizo ya akili ama anawadharau sana anaowadanganya,” alisema akikariri maneno aliyonukuu kwa Mwalimu Nyerere.
Wakati akidhihaki ahadi za wagombea wa Upinzani, yeye binafsi amekuwa akiendelea kumwaga ahadi kila aendako huku akijigamba kuhusu utekelezaji wake.
“Tofauti kati ya ahadi zangu na za kwao ni kwamba wanajua kuwa za kwao ni za uongo na hazitekelezeki na za kwangu ni za ukweli na zinatekelezeka.”
Kwa upande wake Dk. Slaa naye amekuwa akijibu mapigo kwa kusema kwamba Kikwete amekuwa akitoa ahadi nyingi zisizotekelezeka na baadhi ya ahadi nyingine ni zile ambazo zipo katika bajeti ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ambazo zinaweza kutekelezwa na kiongozi yeyote atakayeingia madarakani.
Wakati hayo yakiendelea, tafiti mbili za kura za maoni zilizotolewa na Mpango wa Utafiti na Demokrasia (REDET) na kampuni ya kigeni ya Synovate Limited, zinaonyesha kwamba Kikwete amekuwa akishuka umaarufu huku Dk. Slaa akipanda.
Wakati aliingia madarakani mwaka 2005 kwa kupata zaidi ya asilimia 80, sasa tafiti za REDET na Synovate zimekuwa zikionyesha kwamba Kikwete amekuwa akishuka umaarufu wake kwa kasi huku mwenzake (Dk. Slaa) aliyejitosa katika kinyang’anyiro cha urais hivi karibuni akipanda chati kwa kasi inayotishia hali ya baadaye ya chama tawala.
Katika utangazaji wa matokeo yake, REDET ilidai utafiti wake unaonyesha Rais Kikwete angechagulika kwa asilimia 71.2 kama uchaguzi ungefanyika Septemba, mwaka huu, akiwa ameshuka kutoka asilimia 77 aliyokuwa nayo kabla ya Dk. Slaa kujitokeza kulingana na utafiti uliofanywa pia na REDET Machi mwaka huu.
Katika utafiti huo wa REDET wa Septemba, Dk. Slaa alipewa asilimia 12.3 wakati Profesa Ibrahim Lipumba akipewa asilimia 10.1.
Hali imekuwa tofauti kwa Synovate ambayo kama REDET nayo ilifanya utafiti mwezi huo huo, Septemba.
Utafiti wa Synovate ulibainisha ya kuwa Kikwete angechagulika kwa asilimia 61 kama uchaguzi huo ungefanyika wakati wa utafiti husika, yaani Septemba, mwaka huu. Wakati Kikwete akishushwa na Synovate ikilinganishwa na matokeo ya REDET, Dk. Slaa aliongezwa kwa asilimia takriban nne, akipewa asilimia 16 huku Profesa Lipumba akishushwa zaidi kwa asilimia tano, yaani akipewa asilimia tano kutoka 10 za REDET.
Tafsiri inayojitokeza ya dhahiri ya kura hizo za maoni inatajwa kuwa ni Kikwete kushuka kwa kadiri muda unavyokwenda na siku ya upigaji kura inavyosogea.
Katika hatua nyingine, utafiti wa Synovate umeibua sura nyingine ya kwamba Rais Kikwete anakubalika zaidi kuliko taasisi anazoongoza.
Maoni hayo ni pamoja na ukweli kwamba Rais ndiye anayeteua watendaji wakuu wote wa taasisi za umma nchini.
Katika ufafanuzi wa hali hiyo, kwamba inakuwaje watu waliohojiwa wawe na imani na utendaji wa Rais Kikwete kwa asilimia 84, lakini kwa Baraza la Mawaziri ambalo analiongoza imani yao iwe asilimia 50, Jeshi la Polisi asilimia 45 na TAKUKURU asilimia 46, Mkurugenzi Mkazi wa Synovate Tanzania, Aggrey Oriwo alijibu kuwa; “Hata yeye hali hiyo inamchanganya.”
Aliongeza Oriwo: “Hiyo hata mimi inanichanganya. Sielewi, lakini ndiyo matokeo halisi.”
Huo si utafiti wa kwanza kuonyesha kuwa watu wanaohojiwa wana imani kubwa zaidi na Rais Kikwete lakini si na watendaji walioko chini yake, kuanzia Baraza la Mawaziri na wengine.
Kutoka katika Mikoa ya Rukwa na Katavi, Mwandishi Wetu Felix Mwakyembe aliyekuwa anafuatilia kampeni za CHADEMA anaripoti kwamba kulingana na hali halisi ya kisiasa ilivyo haitakuwa ajabu iwapo chama hicho kitaibuka na majimbo mengi zaidi ya CCM.
Dk. Slaa aliingia mkoani Rukwa Oktoba 5, jioni na kufanya mkutano mmoja wa kampeni kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Chanji iliyo nje ya mji wa Sumbawanga ambapo umati uliojitokeza siku hiyo unaelezwa na wenyeji kuwa ni mara tatu ya ule uliojitokeza kwenye kampeni za mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Pamoja na uwanja wa mkutano wa mgombea huyo kuhamishiwa nje ya mji dakika za mwisho, bado wananchi kutoka kona zote za mji huo pamoja na vijiji vya jirani walifika kwa wingi kumsikiliza mgombea huyo.
Hali ilikuwa hivyo hivyo katika mikutano yake mbalimbali aliyoifanya katika majimbo ya Kwela, Kalambo, Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini kwa mkoa wa Rukwa, Mpanda Mjini, na Mpanda Vijijini.
Kuna mambo kadhaa yaliyowageuza wananchi wa mikoa hiyo kifikra na kimtazamo, na dalili zake hazikuanza kujitokeza mwaka huu; bali takribani miaka minne iliyopita ambapo mbunge anayemaliza muda wake wa jimbo la Mpanda Mjini, Arfi Said wa CHADEMA alipoziona aliwatahadharisha CCM katika mahojiano yake na gazeti moja la kila wiki.
“Kati ya mwaka 2006 na 2007 nilifanya mahojiano na gazeti moja la kila wiki. Nilimwambia mwandishi yule kwamba Rukwa si salama kwa CCM, kauli hii
ilipuuzwa, na sasa haya ndiyo matokeo yake,” anasema Arfi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.
Zinatajwa sababu nyingi kuchangia katika kubadilisha fikra na mitazamo ya wananchi wa mikoa hiyo, lakini za msingi zikiwa wananchi kukata tamaa na ahadi ambazo wamekuwa wakipatiwa tangu Uhuru ikiwemo ile ya ujenzi wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga na Mpanda.
Sababu nyingine inatajwa kuwa ni hatua ya kuwazuia wananchi hao kuuza ziada ya mazao yao nje ya nchi wakati soko lipo wazi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Zambia; huku viongozi wake wakifahamu fika kuwa uchumi wa wananchi katika mikoa hiyo unategemea zaidi kilimo ambacho kimeajiri sehemu takribani wakazi wote wa mikoa hiyo wakiwemo wafanyakazi na wafanyabiashara.
Ni kutokana na umuhimu wa kilimo kwa wakazi wa mikoa hiyo ambapo ufisadi uliofanyika kwenye vocha za pembejeo zenye thamani ya takribani shilingi bilioni sita, ulizidisha hasira zao kwa CCM na serikali yake, na katika hili hakuna mtetezi wa CCM kwenye mikoa hiyo, si wananchi wa kawaida wala wanachama na vigogo wa chama hicho.
“Wananchi waliahidiwa mambo mengi, waliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini hawayaoni. Maisha yamepanda sana, vitu vimepanda bei, hawayaoni yale maisha waloahidiwa,” anasema mgombea ubunge katika jimbo la Sumbawanga Mjini, Mwalimu Norbert Yamsebo.
Wagombea wote wa CCM katika majimbo ya mikoa hiyo ni wapya baada ya wale wa zamani wote kuanguka kwenye kura za maoni ukiacha wawili, Paul Kimiti na Chrisant Mzindakaya, ambao waliamua kustaafu siasa za uwakilishi kwa hiari yao.
Kura hizo za maoni zinaelezwa pia kuchangia katika kubadili fikra za wananchi wa mikoa hiyo, na mmoja wa makada wa chama hicho na mfanyabiashara mjini Sumbawanga anasema:
“CCM walishindwa kudhibiti rushwa wakati wa kura za maoni. Waliopitishwa hawana uwezo, walitumia zaidi nguvu yao ya pesa.
Unapozungumza na wenyeji wa jimbo hilo unabaini jambo moja la msingi, kwao tabia ya mgombea ni sifa ya msingi ili achaguliwe, na hapa ndipo kilipo kikwazo kwa wagombea wa CCM.
“Wana mambo ambayo katika jamii hayastahili, ushahidi upo na mambo yao yako wazi,” anasema mama mmoja katika Kijiji cha Katumba, jimbo la Sumbawanga Mjini.
Kiogozi mwingine mkoani Rukwa anabainisha kasoro kwenye kura za maoni akisema: “Watu wamebadilika sana kifikra kutokana na kura za maoni. Matokeo ya kura za maoni za CCM yalimuacha kila mtu kinywa wazi. Sifa za wagombea wa CCM ni mbaya. Katika suala la maadili hawamo.”
Wakati huohuo, Mwandishi Wetu wa Kanda ya Kaskazini, Paul Sarwatt anaripoti kwamba wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikielekea ukingoni, hofu ya hali ya usalama imetanda miongoni mwa wakazi wa Jimbo la Uchaguzi la Arusha Mjini baada ya kuzuka kwa vurugu zinazohusiana na masuala ya kisiasa katika maeneo kadhaa ya mji zinazodaiwa kufanywa na kikundi cha vijana ambao ni wanachama wa CCM ambao wamepachikwa jina la “Interahamwe” na wananchi.
Interahamwe ni kikundi cha wapiganaji wa kabila la Wahutu nchini Rwanda ambao walihusika sana katika mauaji ya halaiki ya Wanyarwanda zaidi ya 800,000 wenye asili ya Kitutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati mwaka 1994 na kesi za waliohusika na mauaji hayo zinafanyika mjini Arusha katika mahakama ya Umoja wa Mataifa ya ICTR.
Hali ya uslama imeanza kuwa tete kutokana na kuwapo kwa vurugu za hapa na pale zinazohusiana na masuala ya kisiasa katika wiki mbili zilizopita ambapo pamoja na kuzuka kwa kikundi hicho kinachotishia amani, viongozi wa CHADEMA wa Mkoa wa Arusha, Jumamosi iliyopita waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa madai mazito dhidi ya CCM na vyombo vya usalama.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alithibitisha chama chake kuhujumiwa na kikundi hicho ambacho pia kinatishia usalama wa wananchi wengine ambao wameonekana kukiunga mkono chama chake.
“Ni kweli mabango ya wagombea wetu wa nafasi za udiwani, ubunge na urais yameng’olewa katika maeneo ambayo tumefungua mashina mapya na tumetoa taarifa Polisi na kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambao wametuahidi kuwa watafuatilia na kuchukua hatua,” alisema Mwigamba.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa moja ya magari yanayotumiwa na vijana hao ina namba za usajili T 824 AYN lakini magari mengine namba zake hazikuweza kufahamika kutokana na magari hayo kufunikwa kitambaa katika sehemu yenye namba za usajili hivyo kuwa vigumu kufahamu namba zake.
“Inavyoelekea vijana hao ambao wananchi sasa wamewapachika jina la Interahamwe wamekuwa wakifanya uhalifu huo bila kificho huku vyombo vya dola vikishindwa kuchukua hatua kwani kufanya hivyo ni uvunjaji wa sheria,” alisema Mwigamba.
Akizungumzia hali ya usalama, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Basilio Matei, aliiambia Raia Mwema kuwa wanadhibiti vurugu zilizoanza kujitokeza na tayari watu kadhaa walikuwa wanahojiwa kutokana na tuhuma hizo za kujihusisha na kuchana picha za wagombea na kung’oa bendera za vyama.
“Kuna watu watatu tayari wamekamatwa kuhusiana na matukio hayo na wengine tumewahoji lakini niko nje ya ofisi kikazi na siwezi kukumbuka majina yao na maelezo mengine ya msingi ila kama jeshi tunajitahidi kudhibiti matukio hayo ambayo yanaweza kuvuruga amani,” alisema.
Aliongeza Kamanda Matei: “Si rahisi Polisi kuwa kila eneo ambalo kuna mabango ila kama kuna watu wanafanya matukio hayo basi wananchi waripoti haraka kituoni ili hatua za haraka zichukuliwe kwani kwa kufanya hivyo watu hao wanavunja sheria za nchi.”
Kuhusu madai ya CHADEMA kuwa mgombea wa ubunge wa CHADEMA anafanyiwa njama za kumdhuru, Kamanda Matei aliwataka apelekewe malalamiko hayo na ushahidi ili jeshi lichukue hatua.
“ Lakini katika kipindi hiki cha kampeni malalamiko kutoka kwa vyama na wagombea wao ni mengi na hii inatokana na ushindani wa kisiasa uliopo, sisi kama Polisi hatutaki kujiingiza katika malumbano yanayoweza kuleta tafsiri potofu kwa watu kuwa tunapendelea chama fulani, ila tutafuata sheria na kanuni zinazosimamia masuala ya uchaguzi bila kupendelea upande wowote,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Jubilate Kileo, alikanusha taarifa kuwa kuna kikundi cha vijana wa chama hicho kinajihusisha na mbinu chafu za kung’oa mabango ya CHADEMA kwa kueleza kuwa kama chama hawakuwahi kutuma mtu au kikundi cha watu kutekeleza mipango ya aina hiyo.
“CCM haiwezi kufanya mbinu za kipuuzi kama hizo na hayo ni madai ambayo hayana msingi….Sisi tunaelewa fika kuwa kura iko ndani ya utashi wa mtu binafsi, kwa hiyo kung’oa bendera na kuchana mabango haiwezi kusaidia chochote,” alisema Kileo.
Kileo aliongeza: “Kwanza ni kawaida yao CHADEMA kupiga kelele kila mara kuwa wanahujumiwa. Nawapa ushauri kuwa muda wa siasa za kuomba huruma ya wananchi umekwisha, waeleze watawafanyia nini wakazi wa Arusha iwapo watapewa ridhaa ya kuwaongoza badala ya kuzusha mambo yasiyo na maana”.
Kutoka Mwanza Mwandishi Wetu anaripoti kwamba mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa mwaka huu kuwa rais, atafufua kilimo cha zao la dengu katika Mkoa wa Mwanza na kulifanya kuwa zao kuu la pili la biashara baada ya pamba.
Akihutubia katika mikutano ya kampeni iliofanyika katika maeneo ya Kayenze, Pasiansi na Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo, mgombea huyo alisema kuwa zao la dengu ambalo miaka ya nyuma lilikuwa likilimwa kwa wingi katika Wilaya za Misungwi, Magu na Kwimba mkoani Mwanza na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Shinyanga lina soko kubwa nchini India na baadhi ya nchi za Asia.
“Ndugu zangu, wenzetu Wahindi hawali nyama hivyo wanategemea kupata ‘protein’ kupitia mboga za jamii ya mikunde. Na dengu ni chakula kinachopendwa sana na Wahindi. India ina idadi kubwa ya watu hivyo uhakika wa soko upo kwani kuna mahitaji makubwa ya dengu India. Kwa hiyo mkinichagua tutahakikisha dengu inakuwa zao la pili kwa biashara hapa baada ya pamba,” Anaongeza.
Mbali ya kuahidi kufufua zao hilo la dengu ambalo linakaribia kutoweka kutokana na wakulima kukata tamaa baada ya kukosa soko na kutopewa kipaumbele na serikali, Profesa Lipumba anasema atahakikisha uzalishaji wa pamba unaongezeka na mkulima anapata bei nzuri tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo bei ya zao hilo inazidi kuporomoka.
Anaongeza kuwa licha ya serikali kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ‘fidia’ baada ya bei ya pamba kuporomoka kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani, fedha hizo za walipa kodi hazikumsaidia mkulima wa kawaida isipokuwa ziliiishia mfukoni mwa wafanyabiashara na mafisadi na kwamba bado bei ya pembejeo za kilimo ni kubwa hivyo kuwa mzigo kwa wakulima.
Alishangazwa na wakulima wa zao la mhogo katika wilaya za Sengerema na Geita kuuza mhogo nchi jirani ya Uganda ambako hutengenezwa biskuti na kurudishwa kuuzwa nchini wakati inawezekana kuwa na viwanda vya biskuti nchini ambavyo vitakuwa vinanunua mihogo ya wakulima hapa nchini.
Na katika sekta hiyo hiyo ya viwanda, Profesa Lipumba aliwahidi wana Mwanza kuwa atahakikisha kuwa kiwanda cha nguo cha Mwatex kinarejea katika uzalishaji wake wa kawaida hivyo kuongeza ajira kwa wananchi pamoja na kufufua viwanda vingine ambavyo licha ya kubinafisishwa havifanyi kazi na vingine vimegeuzwa kuwa bohari.
Mchumi huyo anasema kuwa mzunguko wa fedha katika jiji la Mwanza unaweza kuwa zaidi ya shilingi milioni 600 kwa siku kutokana na rasilimali zilizopo na kwamba hakuna sababu kwa wakazi wa jiji hilo kulalamika hakuna ajira na huduma duni za kijamii ikiwemo ukosefu wa maji wakati wamezungukwa na ziwa na mito.
Profesa Lipumba alionekana kuwakuna wananchi wa Wilaya ya Geita pale alipozungumzia suala la madini na kusema hakuna sababu ya wao na Watanzania wengine kuendelea kuwa maskini wakati wamejaaliwa utajiri mkubwa wa madini ya aina mbalimbali na kwamba akichaguliwa kuwa rais atahakikisha kuwa kodi ya mrahaba inaongezwa na kuwa asilimia 30 badala ya 3 ambazo zinatozwa hivi sasa na serikali ya CCM.
Anawapa matumaini wananchi kwa kusema kuwa hilo linawezekana kwani nchini Botswana serikali inapata zaidi ya aslimia 60 na kwamba atafuta misamaha yote inayotolewa na serikali kwa wawekezaji wa migodini.
Akizungumza na jamii ya wavuvi katika wilaya za Sengerema na Ilemela, mgombea huyo wa CUF aligusia kilio chao cha siku nyingi cha zana zao kukamatwa kwa madai kuwa ni haramu wakati viwanda vinavyozitengeneza havichukuliwi hatua zozote.
“Wavuvi na wafanyabiashara wadogo wa samaki wananyanyaswa kwamba wanatumia zana ambazo haziruhusiwi na wanavua na kuuza samaki wachanga. Wavuvi wananunua nyavu zilizotengenezwa na viwanda halafu serikali ya CCM inawakamata wao badala ya viwanda vinavyotengeneza hizo nyavu. Serikali inapaswa kuwalipa fidia wavuvi walionunua nyavu ambazo sasa wamezipiga marufuku”, anasema.
Profesa Lipumba pia alizungumzia suala lililoibuka hivi karibuni la mauaji ya walemavu wa ngozi (albino) hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kusema kuwa serikali ya CCM halijalishughulikia ipaswavyo suala hilo kutokana na baadhi ya vigogo ndani ya chama na serikali yake kuamini katika ushirikina.
Anadai: “Mauaji ya Albino yanaendelea kwa sababu kuna baadhi ya vigogo ndani ya CCM na serikali yake wanaamini ushirikina. Sisi tutahakikisha mauaji ya Albino yanakomeshwa na wahusika wote wanakamatwa na kufungwa”.
Mgombea huyo ambaye amemaliza ziara ya kampeni mkoani hapa juzi Jumatatu na jana kwenda mkoani Mara, mbali na kuzungumzia sera za chama chake katika kuboresha uchumi na kuleta maendeleo ya nchi, amekuwa akijikita katika maeneo ambayo wagombea wengine wa urais waliokwishapita hapa hawakuyagusia.
Wagombea urais ambao tayari wameishafika kuomba kura kwa wananchi mkoani hapa ni Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (CCM) Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA) na Peter Kuga Mziray (APPT- Maendeleo).
Tofauti na mikutano ya Kikwete na Slaa ambayo ilihudhuriwa na wananchi wengi na kufanyika kwenye viwanja vikubwa, mikutano ya Profesa Lipumba haikuwa na wananchi wengi sana na ilikuwa ikifanyika katika maeneo ya kawaida kabisa kiasi cha baadhi ya watu kudhani kuwa ni mkutano wa mgombea ubunge au udiwani.
Ukiondoa mkutano wa mwisho aliofanyika juzi jioni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo ambao pia ulitumiwa na Slaa, mikutano mingine alifanya katika maeneo ya kawaida kabisa.
Pia kama ilivyokuwa katika mikutano ya kampeni ya mgombea wa CHADEMA Dk. Slaa, kwenye mikutano ya Lipumba hapakuwa na burudani za vikundi vyovyote vya sanaa ili kuvutia wananchi au kuwezesha wananchi kufika eneo la mkutano kwa kutoa usafiri wa bure kama ilivyo kwenye mikutano ya mgombea urais wa CCM, Dk. Kikwete.
Burudani pekee iliyokuwa ikitolewa katika mikutano ya Lipumba ni kwaya ya chama hicho ambayo hata hivyo ilikuwa ikitumia muda mfupi kuimba nyimbo za kukipigia debe chama hicho na wagombea wake.
Hata hivyo mgombea huyo wa CUF alikuwa na staili nyingine ya kuomba kura kwa wananchi kwa kusimama na kusalimiana nao kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama kwenye masoko au mialo ya wavuvi ambapo hushuka na kusalimiana na mwananchi mmoja mmoja.
Licha ya kuwa hakupata wananchi wengi kama ilivyokuwa kwa Kikwete na Dk. Slaa, bado Profesa Lipumba alionyesha kutumia utaalamu wake kama mchumi pamoja na uzoefu wake wa kugombea nafasi hiyo ya urais kwa mara ya nne katika kujenga hoja kwa kutumia mifano rahisi hivyo kuwagusa wananchi wa kawaida.
Kwa mfano alitumia ongezeko la bei ya bidhaa mbalimbali kuanzia mwaka 2005 na kukua kwa tatizo la ajira hadi watu kuokota chupa tupu za maji kwa ajili ya kuziuza huku serikali ikisema ni wajasiriamali na ni sehemu ya ajira iliyoongezeka tangu mwaka 2005.
Kadhalika mikutano hiyo ya kampeni za Profesa Lipumba ilionekana kuwa ya kawaida isiyokuwa na jazba (tension) miongoni mwa wafuasi wake hivyo kumpa fursa mgombea huyo kunadi sera zake na kujenga hoja ya kwanini wananchi hawapaswi kuendelea kuichagua CCM.
Hata hivyo, wadadisi wa mambo ya kisiasa hapa wanasema kuwa mgombea huyo anazidi kupoteza mvuto kutokana na kugombea vipindi vyote tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini mwaka 1992.
“Mimi nilidhani ni kampeni za mgombea udiwani au ubunge lakini nikaambiwa ni Lipumba ndio anahutubia hapa (Pasiansi) ndio nikaja kumsikiliza maana yake watu ni wachache sana ukilinganisha na wenzake akina Slaa na Kikwete. Inaonekana hana nguvu sana. Hata eneo lenyewe hili walilochagua ni dogo sana kwa mgombea urais kuhutubia, wangeenda angalau Furahisha. Lakini anajua kujenga hoja. Tatizo amegombea mara nyingi sana hivyo wananchi wanaona hana jipya tena”, Suleiman Kassim, mkazi wa Ilemela anasema.
Kadhalika suala la udini bado linakiandama chama hicho kwani baadhi ya wananchi wanasema anachagua maeneo ambayo kuna Waislamu wengi ndiyo anakwenda kufanya mikutano yake ya kampeni.
Hata hivyo kiongozi mmoja wa CUF ambaye anaandamana na mgombea huyo katika kampeni zake alikanusha madai hayo kwa kusema kuwa wamekuwa wakifanya mikutano yao bila kujali kuna waumini wa Kiislamu au madhehebu mengine.
“Hizo ni propaganda za kisiasa tu kwani tangu chama chetu kianzishwe kimekuwa kikidaiwa ni cha kidini, mara ni cha Wazanzibari nakadhalika. Haya madai tumeishayazoea lakini tumekuwa tunapita maeneo mbalimbali kuomba kura bila kujali kuna Waislamu au hakuna. Sisi tunasema tukishinda tutaunda serikali ya umoja wa kitaifa sasa tutapendeleaje Waislamu? Na hatuwezi kuwazuia waislamu kujiunga na chama chetu eti tutaonekana ni chama cha Waislamu. Hivi kuna Waislamu wangapi wako CCM au CHADEMA?” alihoji kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa madai kuwa hakuwa amepata ridhaa ya viongozi wake.
Kuhusu uchache wa wananchi katika mikutano yao anasema: “Sisi hatusombi watu kwa magari na wala hatuna ‘fiesta’ (tamasha la burudani la wasanii) kama wanavyofanya CCM. Wameishagundua hawana mvuto hivyo inabidi watumie mbinu za ziada kupata watu halafu wanajisifu mikutano yao imejaa watu wakati wengine wameenda kupata burudani ya bure. Sisi wananchi wanakuja kwa hiari yao kusikiliza sera zetu. Sisi tunaona tunaendelea vizuri na tunakutana na wananchi wengi kwani kama leo (Jumatatu) tumekuwa na vituo vinane vya kuhutubia na kusalimiana na wananchi”.
Mgombea mwingine wa urais ambaye ameishafanya kampeni mkoani Mwanza ni Mziray wa APPT- Maendeleo ambaye alikuwa akitafuta sehemu ambazo kuna mikusanyiko ya wananchi kama maeneo ya sokoni na stendi za mabasi na kuanza kujinadi lakini akiwasifu wagombea wa CHADEMA na CUF kuwa wanafaa zaidi kuliko wa CCM huku akijiita yeye ni ‘mchezaji wa akiba’.
Mpaka sasa bado upepo wa kisiasa mkoani hapa unaonyesha kuwa vyama vya CCM na CHADEMA vitachuana vikali katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

No comments:

Post a Comment