Friday, January 14, 2011

MSIBA WA MASHUJAA: CHADEMA wailiza Arusha
•  Mbowe atoa tamko zito, ahamasisha maandamano nchi nzima

na Waandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kililiteka tena Jiji la Arusha katika ibada, maandamano na mazishi ya mashujaa wake, ambayo yalifanyika kwa amani bila ulinzi wowote wa polisi.
Polisi pekee waliooekana ni wale tu wa usalama barabarani. Barabara kadhaa za jiji la Arusha zilifungwa, na maelfu ya wananchi walitanda kando ya barabara hizo, kushuhudia msafara wa miili ya marehemu ikitoka chumba cha maiti kuelekea viwanja vya NMC, na baadaye kuelekea eneo la mazishi, USA River alikozikwa Ismaili Omar. Mmoja wa marehemu hao, Denis Michael, atazikwa leo Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Mashujaa hao waliuawa na polisi waliokuwa wanapambana na wafuasi na viongozi wa CHADEMA katika kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika viwanja vya NMC, Januari 5, mwaka huu, kudai marudio ya uchaguzi wa meya wa Jiji la Arusha na naibu wake.
Zizi la Arusha lilizizima kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza kwa kishindo katika ibada maalum ya kuaga miili ya marehemu hao.
Katika ibada hiyo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitoa tamko zito lililolaani vikali mauaji hayo, huku akitangaza maandamano mapya yatakayofanywa na chama hicho nchi nzima yakibeba madai kuu nane likiwamo la kutaka kuitishwe mkutano wa kitaifa utakaofanikisha kuandikwa kwa katiba mpya.
Katika madai hayo, Mbowe alitangaza msimamo mkali wa kutaka mashitaka yote yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa ngazi zote wa chama hicho - wanachama, wafuasi na wananchi wengine wote waliokumbwa na kumba kumba ya Jeshi la Polisi - yafutwe bila masharti yoyote, vinginevyo hawatahudhuria mahakamani tena, hata kama kwa kufanya hivyo kutafanya wakamatwe na kurudishwa tena gerezani.
“Tunasisitiza katika jambo hili kwamba viongozi, wanachama na wafuasi wetu wote waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka haya hawatahudhuria mahakamani tena kuhusiana na kesi iliyofunguliwa dhidi yao, hata kama kwa kufanya hivyo kutafanya wakamatwe na kurudishwa tena gerezani,” alisema Mbowe.
Alitaka kuundwe tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoongozwa na majaji wa Mahakama ya Rufani ili ifanye uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa matukio yote yaliyosababisha IGP Mwema kupiga marufuku maandamano ya amani na mkutano wa hadhara kabla ya Jeshi la Polisi kufanya vurugu zilizosababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia.
Dai lingine ni kutaka Waziri wa Mambo ya Nchi Shamsa Vuai Nahodha na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema wawajibike wajiuzulu. nia.
“Kujiuzulu kwao kutapisha uchunguzi huru na wa kina wa matukio yote yaliyosababisha wananchi wetu kuuawa, mamia kujeruhiwa na mamia mengine kukamatwa bila sababu yoyote na kuwekwa rumande na baadaye kufunguliwa mashtaka ya uongo ya jinai,” alifafanua na kuongeza:
“IGP Mwema, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Andengenye na wale wote walioamuru au kutekeleza amri ya kuvunja maandamano na mkutano halali wafunguliwe mashtaka ya jinai kwa matumizi mabaya ya madaraka na kwa kusababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia.”
Mbowe, ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, aliitaka serikali kuwalipa fidia stahili kwa mujibu wa sheria husika za nchi ndugu na jamaa wa wale wote waliouawa kutokana na vitendo vya polisi na wale wote walioumizwa kwa namna yoyote ile na au kuharibiwa mali zao kutokana na vitendo hivyo.
Pia alisema chama hicho kinataka matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha yafutiliwe mbali, na uchaguzi mpya uitishwe haraka iwezekanavyo, kwani uchaguzi huo ndio chanzo cha mauaji ya wananchi.
“Sheria ziweke wazi wajibu wa Jeshi la Polisi la Tanzania kulinda maandamano ya amani na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na/au ya wananchi,” alisema.
Katika kuhakikisha kwamba madai ya chama hicho yanatekelezwa, alisema chama kimeelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wake mikoani na wilayani kuandaa maandamano ya amani nchi nzima ili kulaani mauaji ya wananchi wa Arusha na kudai utekelezaji wa madai hayo.
“CHADEMA Makao Makuu itatuma maafisa wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo wabunge na wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kushiriki katika maandamano hayo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuyaongezea nguvu na hamasa,” alisisitiza Mbowe.
Alimhusisha pia Rais Kikwete, serikali yake na chama chake, akisema waliandaa mazingira ya damu iliyomwagwa Arusha, kwani kwa mujibu wa Katiba, yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama, na pia ndiye aliyewateua IGP Mwema na waziri Nahodha waliosababisha mauaji hayo. Alisema Rais Kikwete pia alitoa kauli tete katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2010, ambayo ilihamasisha polisi kujipendekeza kwa CCM kwa kuzuia kazi za kisiasa za CHADEMA.
Katika ibada hiyo, maaskofu wa madhehebu ya Kikristu mkoani Arusha walimkemea Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, kwa kuitumia Biblia takatifu kuhalalisha uovu; wakamtaka aache tabia hiyo mara moja.
Huku wakimlinganisha na viongozi mbalimbali wanaotajwa kwenye Biblia waliokuwa wakifanya hivyo kulinda uovu wao, maaskofu hao wakiongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, aliyezungumza kwa niaba wenzake, walisisitiza kwamba wataendelea “kuikosoa serikali na chama chochote kile pindi kinapokosea.”
Kauli ya  Makamba iliyowakera maaskofu hao, na ambayo amekuwa akiirudia mara kwa mara, ni ile aliyotumia  kuwakejeli kwa kunukuu maandiko matakatifu ya Kurani na Biblia akisema “tiini mamlaka iliyo kuu.” Walisema ufahamu wa Makamba ni finyu katika kutafsiri maana halisi ya neno hilo.
Askofu huyo alisema kazi ya viongozi wa dini ni kukosoa maovu kwenye jamii. Alisema wataendelea kufanya hivyo kila inapowabidi bila kujali ni nani au chama gani kimekosea, kwani kazi ya manabii tangu enzi za Biblia ilikuwa pia kuiongoza jamii katika njia nyoofu.
“Kama serikali wameamua kutuvunjia heshima, basi wasimame kwenye majukwaaa kutetea uovu wao, na sisi tutasimama kwa ajili ya kupinga uovu wao, tuone Mungu atamsikia nani. Sisi tunataka uchaguzi wa meya na naibu wake urudiwe, apatikane kiongozi halali bila kuangalia atachaguliwa kutoka chama gani, ” alisema Askofu Laizer.
Kiongozi huyo wa kiroho alielezea kukubaliana na kauli za viongozi mbalimbali zilizotolewa kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo, huku akipingana na ile ya Makamba na Katibu wa CCM  mkoa wa Arusha, Mary Chatanda wanaosisitiza kuwa meya wa jiji hilo alipatikana kihalali na kwa kufuata sheria, na kwamba suala hilo likapingwe mahakamani.
Alisema tabia ya Makamba kurudia lugha hizo mara kwa mara imemuambukiza kwa Chatanda ambaye aliwakejeli maaskofu akitaja wavue majoho na wamfuate kupambana katika uwanja wa siasa, hali ambayo amesema ni kuwakosea nidhamu.
''Maaskofu wamesikitishwa na kauli yake na pia kauli ya Katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Mary Chatanda kuwataka kuvua majoho na kuingia katika siasa kwani ni kuwavunjia heshima,'' alisema askofu Laizer.
Katika ibada hiyo, Sheikh Alawi, akisoma dua, alitangaza rasmi kuwa marehemu hao Omar Ismail na Denis Shirima  wamefariki kishujaa.
Mbali na Mbowe, mazishi hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, na wabunge zaidi ya 18, wakiwamo, Godbless Lema John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), Joyce Mukya (Viti Maalumu), Mustafa Akoonay (Mbulu), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Lucy Owenya (Viti Maalumu), Susan Kiwanga (Viti Maalumu), Anna Komu (Viti Maalumu), Tundu Lissu (Singida Kaskazini), Susan Lyimo (Viti Maalumu), Pauline Gekul (Viti Maalumu).
Nayo mashirika 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct), yamelaani ukiukwaji wa haki za binadamu, demokrasia na uvunjivu wa amani uliosababisha kuumizwa na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia mjini Arusha.
Katika taarifa iliyotolewa jana kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya, wanaharakati kutoka mashirika hayo walisema:
“Vurugu hizo ziliendana na unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia kwa baadhi ya waandamanaji, huu ni ukiukwaji wa haki za msingi za kibinadamu na za wanawake…
“FemAct inalaani kitendo cha halmashauri ya Jiji la Arusha kusimamia na kuendesha uchaguzi batili usiozingatia sheria kanuni na taratibu za uchaguzi ambao ulimpata Meya na Naibu wake 18/12/,2010 na kumpelekea kutokea kwa vurugu hizo.
“FemAct tunalaani kwa nguvu zetu zote ubabe na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi ambacho ni chombo cha ulinzi na usalama wa wananchi kugeuka na kuvunja sheria ya kuwazuia wananchi kutoa sauti zao na kupigania haki zao za msingi…
“Sisi wanaharakati tunalitaka jeshi la Polisi na serikali kuweka wazi muktadha na hali halisi ya tukio la Arusha, kuwataja na kuwachukulia hatua za kisheria walioshiriki kuvunja sheria na kutoa idadi kamili ya wananchi waliojeruhiwa na kupoteza maisha katika tukio hilo.”
Waliitaka serikali kuunda tume huru itakayowashirikisha wananchi, plisi, vyama vya siasa, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kushughulikia suala hili na kuwahakikishia wananchi wa Arusha kuwa tukio kama hili halitatokea tena.
“Tunaitaka serikali,vyama vya siasa na vyombo vya dola kutokuwanyamazisha wananchi, viongozi wa kijamii na dini wanaolizungumzia suala la Arusha kwani hivyo ni kinyume na demokrasia iliyoendelea na kukomaa nchini.”

No comments:

Post a Comment