MGOMBEA wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Monduli kupitia tiketi ya CCM, Edward Lowassa, jana alizindua rasmi kampeni zake akiwa na kauli mbiu ya aina yake kwa wananchi wa Monduli.

Kaulimbiu ya Lowassa ambaye anawania tena nafasi hiyo, ni 'tulifurahi pamoja, tukahuzunika pamoja, tutasonga mbele pamoja na tutashinda.'

Kaulimbiu hiyo, inalenga katika kuzungumzia tukio lililomfanya alijiuzulu nafasi ya uwazi mkuu baada ya kutajwa na kamati maalum ya bunge, kuwa alihusika na kuisaidia kampuni yenye utata ya Richmond, kupata zabuni ya kuzalisha umeme na baadaye ilibainika haikuwa hakuwa na uwezo.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika mji wa Mto wa Mbu, Lowassa alisema katika kipindi chake cha ubunge, ametekeleza kwa asilimia 99 ilani ya chama chake.


"Katika kipindi changu cha ubunge nimetekeleza ilani ya chama vizuri na sasa tunahitaji kuendeleza yale ambayo tumefikia na kubuni miradi mipya ya afya, maji na elimu,"alisema Lowassa.

Mgombea huyo ambaye alikuwa akishangiliwa mara kwa mara kwa wananchi kuimba kaulimbiu yake, alisema anataka katika uchaguzi wa mwaka huu, achaguliwe kwa kura zote na kuhakikisha kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya CCM, Jayaka Kikwete, atapata kura nyingi kuliko majimbo yote hapa nchini.

"Kama mlivyomuahidi Rais, naomba katika uchaguzi huu tuvunje rekodi ili jimbo letu liongoze kwa kumpigia kura nyingi,"alisema Lowassa.

Katika mkutano huo, Lowassa alieleza mikakati kadhaa ya kusaidia jimbo hilo,kama atachaguliwa kuwawakilisha wananchi kwa muhula mwingine wa miaka mitano ijayo.

Katika sekta ya elimu, alisema anakusudia kuwa jimbo hilo linakuwa na shule za sekondari tatuzi za kidato cha tano.

Alisema katika sekta ya maji, akichaguliwa atafanya jitihada za kusambaza maji katika maeneo yote yenye upungufu na kwamba pia atafanya mikakati ya kuwawezesha vijana kupata mikopo.

Mgombea huyo pia alisema kama atachanguliwa, atasaidia upatikanaji wa mikopo kwa wafugaji wa jimbo hilo ili waweze kufuga kisasa.

Lowassa alisema tayari kiasi cha Dola 30,000 za Kimarekani, kimepatikana kwa ajili ya mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole, aliwataka wale wote wanaowania viti vya udiwani na ubunge katika Mkoa wa Arusha, kushughulikia kero za wananchi kama watachaguliwa.

Nangole alisema kamwe CCM haitavumilia kuona viongozi waliochaguliwa na wananchi, wakikaa kimywa badala ya kufuatilia na kutatua kero za wananchi.