Monday, October 25, 2010

Mdahalo ITV Bila Profesa Lipumba Na Wengine, Kwanini?


Ndugu Zangu,
Jana tumesikiliza mdahalo, au labda mazungumzo au mahojiano kati ya Dr Slaa ( CHADEMA) na Rosemary Mwakitwange. Mahojiano yaliyoruhusu wengine kuchangia kwa njia ya simu pia.
Tunawapongeza walioshiriki kufanya jitihada zile. Ilitoa fursa kwa sisi wapiga kura kumsikiliza Dr Slaa. Hata hivyo, pungufu kubwa kabisa lililoonekana ni namna waandaaji walivyoandaa mdahalo wa upande mmoja bila kuwashirikisha wagombea wengine wa Urais waliopitishwa na NEC. Maana, ni vema pia tukatofautisha maana ya mdahalo na mahojiano. Kama yale ya jana yalikuwa ni mahojiano tu, hakuna tatizo kwa mgombea mmoja tu kuhojiwa. Lakini kama unaitwa mdahalo, basi, tujadili maana ya mdahalo.

Kama ni mdahalo, basi, ingekuwa ni vema na busara kwa wagombea wengine wa Urais kushiriki. Bila shaka, wagombea wengine nao wana haki za msingi za kupewa nafasi ya kuelezea sera zao na kujibu maswali ya wapiga kura. Hata kama chama tawala, CCM kimeweka wazi kuwa mgombea wao hatashiriki mdahalo, lakini hatujasikia vyama vingine vitoa misimamo kama hiyo.

Wengi wetu tungependa kuona wagombea wengine wa Urais nao wakialikwa, hivyo basi, kupewa fursa ya kuelezea sera za vyama vyao na kuulizwa maswali. Kungetoa fursa ya wagombea hao kushindana kwa hoja pia. Labda kama kuna maelezo ya kuwa wagombea hao walialikwa lakini hawakuitikia mwaliko wa kwenda studioni. Au kuwa gharama za muda wa kurusha hewani mdahalo ziligharamiwa na chama cha mgombea aliyefika kwenye mdahalo/mahojiano. Kama sivyo, basi, waandaaji watakuwa hawakuwatendea haki wagombea na wapiga kura kwa ujumla wao.

Maana, tukianza sasa kujenga tabia ya kubagua wagombea itakuwa ni jambo la hatari sana. Ikumbukwe, tangu Uchaguzi Mkuu wa 1995, tulianza kujenga misingi mizuri ya wagombea kupewa fursa sawa. Kwenye uchaguzi wa mwaka 1995 wagombea wote wa Urais walialikwa kwenye mdahalo uliofanyika kwenye iliyokuwa Kilimanjaro Hotel. Kama inavyoonekana pichani, kulikuwa na Profesa Lipumba, Augustino Mrema, Benjamin Mkapa na Bwana Cheyo. Historia ni mwalimu mzuri. Tujifunze.

No comments:

Post a Comment