Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa.
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alibadili hali ya hewa mkoani Shinyanga baada ya kuutikisha mji kiasi cha kusababisha bendera za CCM zilizotundikwa kwenye maeneo mbalimbali kushushwa, huku akisema kuwa yuko tayari kunyimwa kura kwa kosa la kulazimisha watoto kwenda shule.Mabasi ya daladala, pikipiki na magari madogo ya abiria (taksi) zinazotoa huduma ya usafiri mjini hapa zilifungwa bendera za Chadema na kufanya usafiri uonekane kama mali ya chama hicho.
Baadhi ya pikipiki ambazo ni maarufu kama bodaboda zilisitisha huduma kwa ajili ya kumsindikiza mgombea huyo wa urais wakati akielekea kuhutubia mkutano wa kampeni.
Jina la Dk Slaa lilitawala mji mzima huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa ikitokea kura za mgombea urais wa Chadema zimezidiwa na mgombea urais wa CCM, wataandamana kwa madai kuwa wanaamini kuwa CCM haipendwi na wananchi wa mkoa huo.
"Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini asiposhinda, basi CCM itakuwa imetenda hujuma kubwa kwa kuwa haina wafuasi na sisi tumeichoka. Chama ni Chadema peke yake ndicho chenye matumaini nasi, CCM imeshindwa kutukomboa," alisema mmoja wa waendesha pikipiki hizo.
Mji wa Shinyanga ulianza kutawaliwa na shamrashamra kuanzia majira ya saa 4:32 asubuhi wakati wakazi walipokuwa wakijiandaa kwenda kumpokea huku mazungumzo ya watu kwenye vikundi mbalimbali yakimuhusu mbunge huyo wa Karatu ambaye ameamua kupambana katika vita ya kuelekea Ikulu.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Joshoni, Dk Slaa aliendelea kuzungumzia matumizi ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete akidai kuwa ametumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kusafiri kwenda Ulaya kunywa chai na kurudi.
Alisema haiwezekani kwa rais anayependa wananchi wake kutumia fedha nyingi kwenda Marekani ambako alidai alipewe nyandarua na rais wa wakati huo, George Bush wakati vyandarua hivyo vinatengenezwa nchini.
Dk Slaa alisema hana ubaya na mwanachama wa CCM bali yeye anapambana na Kikwete, Yusuf Makamba, Pius Msekwa na vigogo wa serikali, kwa sababu hao ndio chanzo cha Watanzania kuishi maisha mabovu yasiyo na mwelekeo.
"Rais wa nchi unakwenda Ulaya kunywa chai kwa kodi za wananchi halafu unarudi kwa kujigamba kuwa umepewa neti za mbu... ni jambo la aibu kubwa. Ameishia kukaa kuzungumzia wawekezaji tu na kusahau kushughulikia masuala ya wananchi, utadhani alipigiwa kura na wawekezaji," alikejeli Dk Slaa.
Alisema kitendo cha Kikwete kuendelea kugharimia uchapishaji wa picha za kampeni ni matumizi mengine mabaya ya fedha, akidai kuwa mgombea huyo wa CCM amekuwa rais kwa miaka mitano na kila mtu anamjua.
"Kwa nini fedha hizo zisitumike kwenye huduma za afya kama kweli wao (CCM) wana uchungu na wananchi wao," alihoji Dk Slaa.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, serikali inayojali wananchi wake ipo radhi kujinyima ili wananchi waweze kunufaika na wawe na maisha mazuri.
Alisema serikali ya CCM imetengeneza wakimbizi wa ndani kwa kuwafukuza wafugaji wa jamii ya Kisukuma ambao sasa wamelazimika kuendelea kulipa faini ya Sh5,000 kwa kila mfugo katika mikoa ya Rukwa, Mbeya na Morogoro.
"Tukipata ridhaa ya wananchi kuongoza nchi, tutarejesha mabwawa yote tuliyoachiwa na wazungu, ili mifugo yetu iweze kupata huduma zote. Hatutaki supermarket (maduka makubwa ya rejareja) zetu ziwe na nyama kutoka nje, wakati uwezo tunao na Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa ufugaji wa ng'ombe," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema Baba wa Taifa, Marehemu Julius Nyerere alisema kuwa ufunguo wa maisha ni elimu, lakini elimu iliyopo sasa ni ya kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ambayo haimsaidii mhitimu kupata ajira.
Dk Slaa alisisitiza mpango wa chama chake wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.
"Afadhali uninyime kura kwa sababu ya kumlazimisha mtoto wako kwenda shule. Lakini sipo tayari kuona watoto wakiendelea kuchunga na kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu," alisema Dk Slaa.
Alisema Chadema inataka kutoa elimu hiyo bure ili kufuta matabaka yaliyopo kati ya walionacho na wasio nacho.
"Dk Slaa alisema taifa halijengwi kwa maneno ya Kikwete majukwaani... kama Kikwete ana uwezo wa kutumia fedha... kusambaza picha bure nchi nzima, kwa nini elimu ishindikane kupatikana bure," alihoji.
"Mwaka huu hadi kieleweke; hakuna wizi wa kura wala nini; sisi wenyewe tutakuwa walinzi wa kura kituo hadi kituo mpaka dakika ya mwisho kwa sababu tuna matumaini makubwa kwamba Dk Slaa Shinyanga anapata kura nyingi kuliko mikoa yote," alisema mmoja wa wananchi waliofurika kwenye mkutano huo alipoongea na Mwananchi.
No comments:
Post a Comment