Thursday, October 21, 2010

Wengi watetea ujasiri wa gazeti Mwananchi

Wengi watetea ujasiri wa gazeti Mwananchi  Send to a friend
Thursday, 21 October 2010 07:35
0diggsdigg
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi John Chiligati
Waandishi Wetu
WASOMI, wanasheria, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida wamepinga tishio la Serikali  kutaka kulifungia gazeti la Mwananchi.Sauti hiyo ya umma imekuja kufuatia kitisho cha Msajili wa Magazeti nchini, kuonya uwezekano wa kulifungia au kulifuta gazeti hili kama halitabadilika kuandika kile alichokiita habari za uchochezi.

Watu hao wa kada tofauti katika jamii wameweka bayana kwamba, bado wanaliamini gazeti hili na wamesikitishwa na kitisho hicho cha Serikali na kutoa shutuma bila kuziainisha na kuziweka wazi.

Kwa nyakati tofauti, wakizungumza katika viunga mbalimbali vya Jiji la Dar es Salaam, waliwapa nguvu wahariri na waandishi wa Mwananchi kutotishika na badala yake waendelee kutoa habari bila upendeleo.

Hata hivyo, baadhi ya wadau walitoa hisia zao kwa kukosoa baadhi ya mambo ya msingi ambayo walidhani kimtazamo, hayaendi vizuri.

Lakini, pamoja na ukosoaji huo wote walikubali kwamba, Serikali haikulitendea haki Mwananchi kwa kutoweka bayana tuhuma hizo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kililaani tamko hilo la Serikali kwa maelezo kwamba, ikitekeleza uamuzi huo itakuwa ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

LHRC katika msimamo wake huo, kimeweka bayana kwamba gazeti la Mwananchi limekuwa likitoa habari za ukweli bila woga na kama ni suala la kufungia chombo cha habari, Serikali ingepaswa kufanya hivyo kwa gazeti la Daily News, ambalo liliandika habari za uchochezi hivi karibuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Francis Kiwanga alisema  wameshtushwa na taarifa hizo za kufungia gazeti hili.

“Ukweli ni kwamba taarifa hizi zimetushtua maana inaonekana dhahiri Serikali inataka kuvunja sheria na kukiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya kutoa maoni, kama kweli serikali ina nia njema basi ianze na gazeti la Daily News vinginevyo ni kutaka kutishia vyombo vya habari,” alisema Kiwanga.

Alifafanua, kitendo kilichofanywa na mhariri wa gazeti hilo la serikali kuwa mgombea wa Chadema hawezi kuwa rais, kinaonyesha moja kwa moja ni habari za uchochezi.

Kiwanga aliongeza kwamba, habari zinazoandikwa na gazeti la Mwananchi ni za ukweli na uhakika na kuitaka Serikali kuthibitisha zile inazoziita za uchochezi.

“Tunawaunga mkono waandishi wa Mwananchi kwa kuwaeleza ukweli hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, maana ni gazeti linalojitegemea bila upendeleo,” aliwapa nguvu waandishi na kuongeza:,

"Napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwapa taarifa wananchi, msiogope vitisho.”

Kiwanga alisema tatizo linalowapa shida viongozi ni kushindwa kutekeleza ahadi wanazozitoa, wakati wa kuomba kura badala yake wanaanza kulaumu baada ya kuhojiwa na wananchi juu ya ahadi walizoziahidi.

Wakati huo huo, wakazi wa Mabibo Manispaa ya Kinondoni walitoa maoni yao juu ya sakata hilo, wakisema hatua hiyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya kupata habari.

Mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Ally Saleh, alisema  kinachoonekana ni Serikali kuchukia kuambiwa ukweli.

“Mimi ni mpenzi wa gazeti la Mwananchi kutokana na habari zake ambazo zimekuwa zinanifurahisha, ndio maana hata sasa hivi nipo nalisoma... Serikali haitaki kuambiwa ukweli... sikubaliani na tamko hili (la kutaka kulifungia),’’alisema Saleh.

Mkazi waMabibo, Joseph John alisema akiwa ni mpenzi wa gazeti la Mwananchi, hajawahi kuona habari zinazoitwa za uchochezi bali analipenda kutokana na habari anazoamini ni za ukweli.

“Ni mara chache kupita siku bila kusoma gazeti la Mwananchi, nawapongeza kwa habari zenu mnazoziandika. Sisi hatuoni habari za uchochezi zinazozungumziwa na Serikali,” alisema John.

 Naye, Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Haron Tairo alisema siku zote msema kweli huwa hapendwi na hivyo hata gazeti liandikalo ukweli haliwezi kukubalika na wote.

“Nimekuwa niki-check mambo mnayoandika hasa kuhusu uchaguzi sijaona tatizo, mmekuwa fair (mkitenda haki) na mnaandika views (mawazo) za watu mbalimbali,” alisema Tairo.Tairo alisisitiza, " Kama wakitaka kutumia haki lazima waainishe makosa yaliyofanywa na gazeti."

“Unaposema mtu amekudhalilisha lazima useme  amekudhalilisha kwa makosa gani na u-justify (uthibitishe).”

Mhadhiri mwingine wa sheria katika chuo hicho, Renatus Mgongo, alisema hajaona tatizo lolote katika uandishi wa habari za gazeti la Mwananchi.

Baadhi ya wakazi wa Muheza wamemtaka Msajili wa Magazeti nchini, kuacha mtindo wa kuvitisha vyambo vya habari hasa magazeti kuwa atavifuta ama kuvifungia kwasababu kufanya hivyo ni kuvinyima uhuru.

Akifafanua zaidi mkazi wa wilayani Muheza, John Said ambaye alidai ni msomaji mzuri wa gazeti hili alisema  Msajili, amekurupuka kuandika barua hiyo ya kutisha vyombo vya habari.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata),  Alhad Mussa Salum alisema anaungana na Serikali juu ya karipio hilo kwa gazeti la Mwananchi.
“Kama Serikali imeona kuna tatizo basi kukaripia ni vizuri zaidi kuliko kuchukua hatua,” alisema Sheikh Salum.
Alifafanua kwamba, “Sisi sote ni wadau wa amani, vyombo vya habari, Serikali na hata viongozi wa dini, hivyo kukumbushana ni jambo jema na la kawaida kwani Mwananchi ni gazeti linalosomwa na wengi ndani na nje ya nchi.”
Ingawa hakutaja tarehe, Sheikhe Salum alisema, “Zipo baadhi ya habari zinazochapishwa na gazeti la Mwananchi zinaonyesha zina mwelekeo wa uchochezi ingawa sio nyingi.”
Naye, Katibu wa Kutetea Haki za Waislaamu Sheikhe Ponda Issa Ponda, alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mwananchi imeonekana kuegemea zaidi upande wa Chadema kuliko vyama vingine.

“Mwananchi limejikita kwa Dk Willibrod Slaa na linaonekana kama linampiga vita Rais Jakaya Kikwete, lakini hata hivyo, hili karipio ni kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi," alitoa maoni yake.
Tamwa yawapa waandishi
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa,  Ananilea Nkya amelitaka gazeti la Mwananchi  kutoogopa vitisho vya Serikali bali liendelee kuwahabarisha wananchi bila ya upendeleo wowote kama ambavyo limekuwa likifanya.

Nkya mmoja wa wanaharakati nchini ambao chama chake nacho kimeonywa na Serikali kuacha siasa bali kijikite kusaidia waandishi wanawake,  alisema Serikali  ikilifungia gazeti la Mwananchi itakuwa ni uonevu wa wazi kwani  hakuna malalamiko yoyote yaliyotolewa na vyama vya kisiasa au watu wengine kuhusu gazeti hilo.

“Serikali ingekuwa na hoja, ingeeleza wazi kuwa ni habari zipi zilizoandikwa na Mwananchi, ambazo  zimekwenda kinyume na maadili ya uandishi wa habari," alisema.

Aliongeza kwamba  katika barua  zilizoandikwa kwa gazeti hilo kutoka wizara ya habari hakuna hata moja inayoonyesha kuwa uchochezi gani ulioandikwa kupitia gazeti hilo.

Nkya alisema Mwananchi limesimamia ukweli na halijaegemea upande wowote ule kwa kuonyesha lipo chama gani, hivyo kutishiwa kufungiwa ni uonevu uliopo wazi amba kila mtu anauona
Misa Tan yalaani
Naye Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Ayoub Rioba, alisema kamwe wadau wa habari nchini hawawezi kuona Serikali inajaribu kufunga mdomo vyombo vya habari.

Rioba ambaye pia ni, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tayari amewasiliana na Sekretarieti ya Misa, Jukwa la Wahariri pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ili kwa pamoja wakutane na kulitafakari sakati hilo na kisha kutoa tamko la pamoja.
“Siwezi kukuambia ni lini hasa tutatoa tamko hilo, lakini tutalitoa haraka sana,” alisema Rioba na kufafanua:
“Hatuwezi kuvumilia kuishi katika nchi inayoamini demokrasia, halafu inaingilia uhuru wa vyombo vya na kutoa vitisho. Kuna vyombo vinajulikana kuwa vinaandika mambo ya ovyo havitishiwi, lakini, vile vinavyoonekana kuheshimu maadili ya uandishi na haviwezi kuwekwa mfukoni, Serikali inavitishia.”

CCT yasikitishwa na kauli ya Serikali
Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kikirsto Tanzania (CCT), Leonard Mtaita, alisema baraza hilo limesikitishwa na taarifa za Serikali kutishia kufungia gazeti hili.

“Mwananchi ni kati ya magazeti yanayoandika habari zake kwa uwazi na bila upendeleo, sijui msingi wa tangazo hilo la Serikali,” alihoji Mtaita.

Kwa mujibu wa Mtaita, kitendo cha Serikali kutotaja habari inazozilalamikia, zinafanya wananchi waamini kuwa karipio hilo lina msukumo wa kisiasa zaidi.

“Kama wasipokuwa bayana, sisi tutaendelea kuamini kuwa, hayo ni maoni ya chama fulani ama mtu binafsi,” alisema Mtaita. Hata hivyo, aliitaka jamii kuendelea kuwa na imani kwa vyombo ya habari na kuitaka Serikali kuacha kutoa vitisho kwa vyombo vya habari.

Udasa wadai Mwananchi ni makini
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamewataka wafanyakazi wa Mwananchi kutoogopa vitisho vya Serikali bali waendelee kuwahabarisha wananchi bila ya upendeleo wowote kama ambavyo limekuwa likifanya.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, (Daruso), Makuri Pongo, alisema jamii ya wanafunzi katika chuo hicho wamekuwa wakilisoma gazeti hilo kwa sababu ya kuandika habari zilizofanyiwa utafiti.

Pongo alisema kama Serikali ingekuwa na hoja ingeeleza wazi kuwa ni habari zipi zilizoandikwa na Mwananchi, ambazo ni zimekwenda kinyume na maadili ya uandishi wa habari.

“ Mbona kuna gazeti liliandika kwenye tahariri yake kwamba mgombea urais wa chama fulani hawezi kushinda na kuwa rais, hivi msajili wa magazeti alichukua hatua gani dhidi ya gazeti hilo? Huo ni uonevu wa hali ya juu,” alisema.

Alifafanua kwamba, kama Serikali imeshindwa kutaja kosa maalum lililofanywa na gazeti, inaonyesha jinsi baadhi ya viongozi wanavyofanya kazi kwa ajili ya kuwafurahisha vigogo.

Mbeya waasa watendaji kuwa makini
Nao baadhi ya wakazi wa Mbeya walisema  wanasikitishwa na vitisho vya Serikali dhidi ya gazeti la Mwananchi na kwamba, kitendo hicho  kinaonyesha dhahiri viongozi wa  hawatambui majikumu yao.

“Hapa lazima kama wananchi tuihoji  hii Serikali yetu kwa sababu kama gazeti linaandika habari ambazo zina upotoshaji hata sisi wananchi tungeona kwani ndiyo wasomaji, lakini katika hili la Mwananchi hatujaielewa kabisa Serikali,” alisema John Mwanyanji mkazi wa Mwanjelwa.

Alisema ni vigumu kwa mwananchi kuelewa makosa ambayo gazeti la Mwananchi hivyo ni vema Serikali ikatoa ufafanuzi ikiwa ni pamoja na sababu za kutoa vitisho hivyo ili wananchi ambao ndiyo wanasomaji waweze kuielewa Serikali yao  wanayoiamini.

Zawadi  John Mkazi wa Uhindini jijini Mbeya alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi, Serikali ilipaswa kufanya mambo yake ya kiserikali na siyo kuingilia mambo ya kisiasa kwani kufanya hivyo ni kuonyesha kuwepo kwa upendeleo wa moja ya chama cha siasa .
Wanasiasa waponda tishio la Serikali
Baadhi ya wanasiasa nchini nao wameponda kitendo cha Serikali kutishia kulifunga au kulifutia usajili gazeti la Mwananchi.CCM kwa kupitia msemaji wao, ilieleza kwamba haijawahi kulalamikia habari za chama hicho zilizoandikwa kwenye gazeti hilo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), John Chiligati alisema kuwa chama hicho hakijawahi kulalamikia habari zinazoandikwa na Mwananchi na kusisitiza ni sheria ndio itakayotoa jibu.

“Mwananchi! sidhani kama kuna siku mliaandika habari njema kuhusu CCM, ila pamoja na hayo hatujawahi kulalamika, wananchi ndio watakao tuhukumu,”alisema Chiligati

Aliongeza, “Endeleeni hivyo hivyo, lakini suala lenu ni la kisheria zaidi kama mna makosa au hamna makosa sheria ndio itaongea.”

Chiligati alisema vyombo vya habari nchini vinafanya kazi kwa kufuata sheria na kuongeza kwamba, linapotokea tatizo katika vyombo vya habari zipo sheria za kulimaliza tatizo hilo, aidha kufungiwa kwa chombo husika au kufutiwa usajili.

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alifafanua kuwa gazeti la Mwananchi linaandika habari za ukweli bila kuegemea upande wowote ila ukweli huo unaweza kugeuka ubaya hasa kwa watu wanaolengwa.

“Kuna madai kuwa kuna karatasi za kupigia kura zimeingia nchini zikitokea Afrika Kusini ambazo zina alama ya ‘tiki’kwa mgombea fulani, sasa habari kama hii ikifuatiliwa na kuhakikiwa ikitolewa katika vyombo vya habari utasema ni ya uchochezi,”alihoji Mtei.

Mgaya: Tusizibwe mdomo
Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya alisema  kitendo hicho ni sawa na kuziba mdomo wananchi.

Mgaya alisema binafsi hajawahi kuona habari ya upendeleo na kwamba  kwa mtazamo wake Mwananchi ni gazeti pekee lisilopendelea upande wowote hasa wakati huu wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Habari hii imeandikwa na Gedius Rwiza, Petro Tumaini, Fredy Azzah, Raymond Kaminyoge, Geofrey Nyang'oro, Hussein Issa, Beatrice John, Salim Said, Steven William, Muheza

No comments:

Post a Comment