Monday, October 25, 2010



NITAGOMBEA KIPINDI KIMOJA – Slaa
Mwandishi Wetu
(Pichani Dk. Slaa akihutubia maelefu ya wananchi wa mji wa Mwanza siku ya Jumatano)

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa amesema kuwa endapo wapiga kura watamchagua kuwa Rais wao basi atawatumikia kwa kipindi kimoja na hatogombea tena mwaka 2015. Dr. Slaa ametoa ahadi hiyo alipozungumza na kijarida hiki mapema wiki hii katika mazungumzo ya kina yaliyohusu kampeni yake, mipango yake na mwelekeo wa chama chake kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA amesema kuwa tangu mwanzo alipoombwa kuwa mgombea wa Urais katika uchaguzi huu alishaamua kuwa akipata nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa kisiasa nchini basi hatotaka kugombea tena kipindi cha pili akimaliza muda wake wa Urais. Dk. Slaa alirejea maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere Ikulu “siyo mahali pa kukimbilia” na kuwa yeye hakuwahi katika maisha yake kuwazia wala kutamani cheo hicho, hivyo anataka kuingia kufanya aliyoahidi kufanya na kutoka kuwaachia wengine.   

“Tangu mwanzo waliponiomba nilikubali nikiwa na nia ya kuwa Rais kwa awamu moja tu na kinyume na wengine sitoingia ili nitumie miaka miwili au mitatu kujifunza halafu nirudi kuomba niongezewe muda, mimi ninaingia tayari kufanya kazi kwani Urais hauna chuo” amesema Dk Slaa mara baada ya kumaliza mkutano wake mkubwa wa kampeni huko Shinyanga na akiwa anajiandaa na mikutano ya Mwanza na maeneo mengine nchini huku siku zikiwa zinakimbia kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 31 mwaka huu.

Akizungumzia kwa kina uamuzi wake huo Dr. Slaa amesema kuwa pamoja na kuzingatia usia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere yeye mwenyewe alikuwa na sababu zake nyingine za kutotaka kugombea tena kipindi cha pili. “Kwanza, kiumri nitakuwa nakaribia miaka sabini ifikapo mwaka 2015 (Dr. Slaa anatimiza miaka 62 Oktoba 29)  sasa heka heka za kampeni tena na mambo ya kisiasa nataka niwaachie wengine ili na mimi nifurahie maisha ya kustaafu” ameelezea.

Pamoja na sababu hiyo Dr. Slaa ameelezea vile vile nia yake ya kuhakikisha kuwa utakapofika mwaka 2015 serikali ya Chadema na chama vitakuwa vimeandaa watu wa kutosha na wenye uzoefu wa kutosha kiuongozi ili waweze kuchukua nafasi baada  yake. “Unajua CCM wamewaandaa watu wao mbalimbali kiasi kwamba wana wigo mkubwa sana wa kupata viongozi wa serikali kwani wengi wamepata uzoefu wa aina mbalimbali kwa muda mrefu. Kwa upande wetu ninataka tutumie miaka hiyo mitano kuandaa viongozi wapya kabisa wa kisiasa nchini nje ya wale walioko CCM ambao wanaweza kuiongoza serikali.”

Pamoja na sababu hiyo Dk. Slaa amesema kuwa lengo lake ni kuanzisha mabadiliko makubwa nchini ya kusahihisha makosa ya utawala wa CCM yaliyodumu kwa miaka 49. “Ni lazima tusahihishe makosa haya, hatuwezi kuendelea na njia ambayo tunajua tayari tumepotea. Tutakuwa ni watu wa ajabu kama pamoja na kujua tumepotea tutaendelea kwa hiari yetu kuchagua kupotea miaka na miaka, hivyo nataka niweke msingi wa mageuzi makubwa ya utendaji kazi na utawala nchini ili tuweze kuwarithisha watoto wetu na watoto wa watoto wetu taifa bora zaidi lenye mafanikio na maendeleo zaidi”

Akizungumzia mwelekeo wa kampeni yake ambayo kwa maoni ya watu wengi inaonekana kuwa na uhai wa aina yake Dk Slaa amesema kuwa kama kuna watu walifikiri ameingia katika kinyang’anyiro hicho ili kubahatisha basi wamefanya makosa. “Tumeingia kwa lengo la kushinda na siyo kusindikiza na kinachosimama kati yetu na ushindi ni wapiga kura!” Alisema kwa kujiamini. Akijibu swali la ni kitu gani kimemgusa hasa katika kampeni zake zilizomchukua katika kona mbalimbali za nchi yetu Dk. Slaa amesema kuwa kati ya mambo ambayo yamemgusa zaidi na kumfanya awe shime zaidi ya kuwatumikia Watanzania kama Rais wao ni hali ya makazi ya wananchi wengi kijijini.

“Wananchi wetu wengi wanaishi katika nyumba ambazo kwa kweli kabisa hazistahili kuishi wanadamu. Yaani miaka 49 ya uhuru bado watu wanaishi kama walivyoishi kabla ya uhuru na kabla ya kuja wakoloni!, hii ni dhambi ya taifa na ni aibu” alisema Dr. Slaa.

Katika mazungumzo hayo Dr. Slaa amewataka Watanzania kumchagua kwa kura nyingi na wasitishwe na kauli zenye kuwafanya wahofie kupiga kura au kutoona umuhimu wa kura bali wajitokeze kwa maelfu, wakishikana mikono katika familia kwenda kumchagua yeye pamoja na wagombea wote wa Ubunge na Udiwani ili aweze kweli kupata watu wa kushirikiana nao na wenye mtazamo mmoja.

Dr. Slaa amezungumzia mambo mengine mengi kuhusu kampeni yake, ajenda yake na malengo yake kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mazungumzo hayo
na Dr.
Slaa yatarushwa siku ya Jumamosi asubuhi (saa za Marekani) kupitia mtandao wa http://www.bongoradio.com na baadaye yatapatikana kwa njia ya mtandao na Cds yakijumuisha mahojiano na wagombea wengine wa Uchaguzi huu.

No comments:

Post a Comment