04 October 2010
Mussa Juma, Arusha
WAGOMBEA wote wa viti vya ubunge na udiwani kupitia tiketi ya Chadema katika Jimbo la Arusha, jana waliandamana kwenda ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Arusha, wakiilalamikia taasisi hiyo kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya rushwa, walivyodaiwa kuwa vimekuwa vikifanywa na wagombea wa CCM.
Tukio hilo la aina yake, lilisababisha kazi katika ofisi za Takukuru, kusimama kwa zaidi ya saa mbili, kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.Shughuli katika ofisi hizo zilirejea katika hali ya kawaida baada ya kuwasili kwa polisi na kuwatawanya wagombea hao na wapambe wao.
Wakizungumza na ofisa mmoja wa Takukuru ofisni hapo, wagombea hao wakiwa na jazba, waliiomba taasisi hiyo sasa kutamka kuwa imeshindwa kudhibiti rushwa, ndani ya CCM.Mgombea wa ubunge, Godbless Lema, alisema mara kadhaa wametoa taarifa kuwa wagombea wa CCM, wako katika eneo fulani, wakigawana fedha lakini taasisi hiyo, haiendi kuwakamata.
"Juzi tu mimi mwenyewe nimewapigia simu kuwa kuna nyumba moja huko Ngulelo, watu wanagawana rushwa. Katika hilo tulipenyeza mtu wetu, lakini kuanzia saa 12 jioni Takukuru hawakuone hadi saa mbili ndipo walikwenda na kukuta tayari wametawanyika," alisema Lema.
Alisema Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa katika Kata ya Sombetini, aliwapa taarifa kuwa kuna watu wanagawiwa fedha na sukari usiku katika kampeni za nyumba kwa nyumba za CCM, lakini pia hakuna hatua zilizochukuliwa.
"Hata mke wangu juzi kaja hapa tena na usafiri na kuwaambia awapeleke kuna sehemu rushwa inagawanywa lakini hawakwenda. Sasa kama mmeshindwa tuambieni sisi tutajua la kufanya,"alisema Lema.
Wagombea wa udiwani, Estomii Malla wa Kata ya Kimandolu na John Bayo wa Kata ya Elerai, walidai kuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu rushwa inavyotolewa lakini wanashangaa Takukuru, kushindwa kuchukua hatua.
"Tumekuja hapa kusema wazi kama hamuwezi kupambana na rushwa tuambieni, tutaueleza umma na watajua cha kufanya…mbona wakati wa kura za maoni ndani ya CCM mliweza sasa mnashindwa,"alihoji Malla.
Baada ya malumbano hayo, ofisa mmoja wa Takukuru aliomba kukutana na mgombea mmoja mmoja ndani ya ofisi yake, lakini wagombea hao walipinga na kutaka kila mgombea aandamane na wanahabari.
"Sasa mimi nasema siwezi kuwasiliza wote kwanza kamanda wa mkoa hayupo na kama mnasisitiza waandishi siwezi kuwasikiliza kwani kila ofisi ina utaratibu wake,"alisema Afisa huyo.
Hata hivyo baada ya malumbano ya muda, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwambeji, aliingilia kati na kuwataka wagombea hao kuchagua mwakilishi mmoja na kutoa malalamiko pasipo waandishi wa habari.
Baada ya hoja hiyo, wagombea hao, walimteua Lema kuonana na ofisa huyo ili kuwapangia siku ya kuonana na kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Arusha, Ayoub Akida.
Akizungumza mara baada ya kukutana na ofisa huyo, Lema alisema wameshindwa kuafikiana kwani badala ya kuwapangia siku ya kukutana na Kamanda wa Takukuru, alimtaka kuandika malalamiko.
Tuesday, October 5, 2010
CHADEMA waandamana wakiilalamikia TAKUKURU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment