Matokeo ya urais ndani ya siku moja | Send to a friend |
Friday, 08 October 2010 07:22 |
0diggsdigg Hussein Issa na Beatrice JohnTUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imepania kuweka rekodi baada ya kueleza kuwa itatangaza matokeo yote ya uchaguzi mkuu siku moja baada ya kupiga kura, uamuzi ambao unaweza kupunguza mianya ya kuchakachuliwa kwa matokeo ya uchaguzi. Iwapo itatekeleza azma hiyo, Nec itakuwa imeandika historia baada ya kushindwa kutangaza matokeo mapema tangu uchaguzi unaohusisha vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1995. Nec imekuwa ikichelewa kutoa matokeo kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mawasiliano na ukosefu wa teknolojia, hali iliyoweka uwezekano wa matokeo ya uchaguzi kuchezewa, lakini jana ilieleza kuwa hali sasa imebadilika. Mkurugenzi wa uchaguzi wa Nec, Rajabu Kiravu alisema jana kuwa baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika kura za wagombea urais ndizo zitakazopewa kipaumbele katika kuhesabiwa zikifuatiwa na za wabunge na madiwani. Kiravu aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wasimamizi wa kura watatakiwa kutoa taarifa mapema kwa vyama husika kuelezea mahali, tarehe na muda wa kujumlisha kura ili kusitokee malalamiko yoyote. “Wote mnafahamu kuwa kuna sababu za kufuata sheria na taratibu za uchaguzi, ikiwa pamoja na maadili ya tume, hususan kipindi hiki hivyo nina hakika hamtatuangusha kwa kusikia malalamiko ya vyama vya siasa kama ilivyo kawaida,” alisema. Katika baadhi ya chaguzi zilizopita, kwenye baadhi ya maeneo watu walikuwa wakiendelea kupiga kura huku matokeo yakitangazwa, jambo ambalo huathiri wapiga kura. Mwaka 1995, uchaguzi kwenye majimbo ya Dar es salaam ulirudiwa na kusababisha matokeo ya uchaguzi kuchelewa. Kiravu alisema idadi ya wapigakura ni 19,686,608 na vituo vya kupigia kura vitakuwa 51,732 katika mikoa yote. Akizungumza na wasimamizi wa uchaguzi kutoka mikoa yote nchini aliwaambia kuwa wanatakiwa kuhakiki orodha hiyo ya wapiga kura na kama ina kasoro yoyote watakayoibaini wawasiliane mara moja na Nec. Kuhusu ulinzi wakati wa uchaguzi, Kiravu alisema tume imeshahakikisha kuwepo kwa hali ya usalama katika vituo vya kupiga. “Askari watakaosimamia uchaguzi wanatakiwa kutoka katika maeneo yao wanayofanyia kazi na sio kutoka eneo jingine,” alisema. Pia aliwataka wasimamizi kuhakikisha wamepokea orodha ya mawakala na vituo walivyopangiwa kufanya kazi toka kwa viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya husika siku saba kabla ya uchaguzi. “Uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa havizingatii utaratibu uliotolewa na tume kwa visingizio mbalimbali,” alisema Kiravu. Pia awaliwataka wasimamizi hao kutembelea vituo vya kupigia kura kuona hali halisi ilivyo ili kuona kama majengo yapo katika hali salama na kama hakuna majengo ya kudumu, utaratibu wa kujenga mahema ufanyike haraka. “Ni vyema tume ikapewa taarifa mapema kama kuna kituo chochote cha kupigia kura hakifikiki kwa urahisi ili hatua za haraka zifanyike kutatua tatizo hilo,” alisema. Naye mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame alisema sehemu kubwa ya maadalizi ikiwemo uchapaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ugawaji na usafirishaji wa vifaa mbalimbali vya uchaguzi, imekamilika. Aliwataka wasimamizi kutembelea maeneo mbalimbali zinakofanyika kampeni ili kuona namna zinavyoendeshwa na kama zinafuata taratibu zilizowekwa ikiwemo sheria, kanuni na madili ya uchaguzi. Jaji Makame alisema tume itafanya mikutano na vyama vya siasa ngazi ya mkoa Oktoba18 hadi 22 mwaka huu kwa upande wa Tanzania na Oktoba 27 kwa Zanzibar. Kwa mujibu wa Makame, tume itatoa taarifa ya maandalizi ya uchaguzi mkuu na kujadiliana na wadau hao juu ya masuala mbalimbali ya uchaguzi katika maeneo yao. “Kinachotakiwa ni kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa bila mapungufu yasiyo ya lazima na pia mchakato mzima unafanyika kwa uwazi,” alisema Makame. |
No comments:
Post a Comment