Rais anayebeba watuhumiwa hafai
Alikuwa na maana kwamba, kawaida wahalifu huogopa sana mamlaka pamoja na vyombo vya kusimamia sheria na haki.
Wakati huohuo, mamlaka na wote wanaosimamia haki, hutaka na hasa hupaswa, kukaa mbali na watuhumiwa wa uhalifu wowote; kwa maana ya kutokuwa maswahiba.
Lakini sivyo ilivyo kwa mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Amiri Jeshi Mkuu.
Katika kampeni za kugombea urais zinazoendelea nchini kote, Kikwete
ameonekana kwenye majukwaa ya siasa, akikumbatia na kukumbatiwa na watuhumiwa wa makosa makubwa ya jinai nchini.
Hivi tatizo ni la mgombea au watuhumiwa wenyewe?
Polisi mwadilifu, kama raia mwema na kiongozi safi, hapendi kuzoeana na wahalifu; na ndiyo sababu ifanyayo watuhumiwa wa uhalifu kudundwa na moyo kila waonapo walinzi wa sheria na haki.
Sasa inakuwaje rais azoeleke kwa watuhumiwa kwa kiwango cha kuwakumbatia jukwaani na kuwaliwaza kwa lugha nyororo?
Rais anapeleka ujumbe gani kwa wananchi ambao walikuwa wakidhani kuwa kweli kuna vita vya kupambana na wahalifu?
Hivi karibuni jijini Mwanza, nilikutana na Alfred Tibaigana, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Niliongea naye na kumpa pole kwa uchovu kutokana na kinyanganyiro cha kura za maoni katika jimbo la Muleba Kusini ambako aligombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mazungumzo yale, na katika hali ya utani, akanieleza kuwa mpinzani wake mmoja alikuwa anawashawishi wapigakura wasimchague kwa kuwa yeye ni “polisi na hivyo akichaguliwa, “hamtakaa tena mnywe gongo.”
Alisema haamini kuwa kushindwa katika kura za maoni kulitokana na yeye kuwa polisi, lakini hata hivyo anasema, “watu wengi vijijini bado wanaogopa polisi.”
Si kawaida kuona watu wakimzoea polisi hata kama hawana makosa ya jinai. Polisi huitwa kwa majina mengi mabaya na hasa kama wanatimiza wajibu wao sawasawa.
Mahali popote polisi walipo, wahalifu hawana raha. Mahali pengine mijini na vijijini, watu hawapendi kuishi mtaa mmoja na polisi kwa hofu tu kwamba, polisi hawana urafiki wa kudumu. Kimsingi hakuna polisi mwungwana linapokuja suala la uhalifu.
Kama polisi anaweza kuogopwa kiasi hicho, mbona rais, amiri jeshi mkuu na kiongozi wa chama kizee na kikubwa haogopwi na watuhumiwa?
Ingawa ni kweli kwamba vikao vya uteuzi vya chama vilipitisha baadhi ya watuhumiwa kuwa wagombea ubunge na udiwani, haina maana kuwa mgombea wa CCM, ambaye ni rais aliyeko marakani, awe na mazoea na watuhumiwa.
Akiwa mkoani Iringa, Kikwete alimpandisha jukwaani Fredrick Mwakalebela, mwanachama wa CCM anayekabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani kutokana na mchakato wa uchaguzi ndani ya chama cha mgombea urais.
Vyombo vya habari vimeanika habari hiyo. Vikatoa hata picha ya wawili hao wakiwa wameshikana mikono.
Hili ni pigo kubwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU); lakini limesababishwa na Kikwete ambaye kimsingi ndiye kamanda mkuu wa TAKUKURU.
Tangu siku hiyo, inabidi taasisi hii ya kupambana na rushwa ijiulize mara mbili inaposhughulika na Mwakalebela.
Wakati naandika makala hii, afisa mmoja wa TAKUKURU ameniambia, “Rais anatukatisha tamaa” na ndiyo maana hata baadhi ya maafisa wa TAKUKURU nao wameanza kushawishika kupokea rushwa kwani wanaona hawana kamanda aliyedhamiria kukomesha rushwa nchini.
Hata ndani ya jeshi la polisi, askari wa vyeo vya chini wanalazimika “kumalizana na wahalifu” kwa sababu wakikomaa nao hadi vituoni, kuna hatari ya kuwaona wahalifu wakikumbatiana na makamanda wao na kutakiana heri na afya njema.
Akiwa mkoani Kilimanjaro, Kikwete alimnadi Basil Mramba, mtuhumiwa anayekabiliwa na kesi mbaya ya matumizi mabaya ya madaraka na kesi hiyo inaendeshwa na TAKUKURU na mwendesha mashtaka wa serikali.
Kikwete amenukuliwa akasema “anamwamini” Mramba na kuwa ni “mzee kijana” mwenye uwezo mkubwa na maono.
Alipoingia mkoani Arusha akapanda jukwaani na Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzuru na kumnadi kuwa ni mtu safi na “anamwamini” na kuwaomba wananchi wampigie kura kwa sababu “yaliyopita si ndwele.”
Lowassa alijiuzuru kutokana na kashfa ya Richmond iliyojaa matumizi mabaya ya madaraka na harufu ya rushwa.
Bunge la Jamhuri lililomthibitisha alipoteuliwa kuwa waziri mkuu, ndilo lilimchunguza na kumwacha ajiuzulu kwa kashfa hiyo.
Mpaka leo, wananchi wengi wanaamini kuna mengi yanafichwa kuhusu kashfa ya Richmond. Kumnadi Lowassa jukwaani, kama alivyonadi watuhumiwa wengine, kumethibitisha, kwa namna ya pekee, kuwepo kwa uswahiba kati ya Kikwete na ufisadi.
Alipoingia madarakani na kuanzisha operesheni maalum ya kutokomeza ujambazi nchini, Kikwete alichekwa na majambazi wakubwa kwa kuambiwa “unataka kukata tawi ulilolikalia.”
Haukupita muda mrefu, polisi wakiwa katika upekuzi ndani ya nyumba ya mtuhumiwa wa ujambazi, walikuta picha kubwa ya Rais Kikwete akiwa na mtuhumiwa huyo.
Picha hiyo ilipigwa siku mtuhumiwa alipokabidhi hundi ya Sh. 40 milioni zilizotumika katika kampeni ya Kikwete mwaka 2005.
Kilichofuata baada ya hapo ni mtuhumiwa kupewa onyo, kwamba awe mwangalifu na asijihusishe tena na ujambazi.
Haijulikani mamilioni hayo ya shilingi yalitokana na “shughuli” ipi – damu za raia walionyang’anywa magari yao na kuuawa, wakiwemo polisi waliokuwa wanalinda raia hao?
Kikwete ndiye anayejua. Lakini la muhimu ni kwamba urafiki kati ya jemedari Kikwete na watuhumiwa umewaponza wengi.
Inapotokea kamanda anacheka na kukumbatiana na watuhumiwa, askari walio msitari wa mbele wanavunjika moyo na hata maisha yao kuwa hatarini.
Taifa liko vitani dhidi ya rushwa, ubadhilifu wa mali ya umma na hata matumizi mabaya ya madaraka. Katika vita hivi, ni vema itikadi za vyama zikawekwa pembeni na kuweka utaifa mbele.
Maafisa wa TAKUKURU wanapomtuhumu mtu au kumfikisha mtuhumiwa yeyote mahakamani, wanafanya hivyo kwa niaba ya rais.
Sasa inakuwaje rais huyohuyo acheke na kukumbatiana na watuhumiwa jukwaani? Inakuwaje awainue mikono, aseme anawaamini na kuwaombea kura kwa wananchi?
Mapema mwanzoni mwa utawala wake, Kikwete aliwateua kuwa mawaziri watu wa namna ya Andrew Chenge na Mramba hata kama kulikuwa na kelele na manung’uniko mengi kuhusu uadilifu wao.
Ilioekana hilo lilitosha, lakini yaelekea sikio la kufa halisikii dawa. Baada ya hapo Kikwete aliendelea kuwateua, katika nafasi mbalimbali, maafisa waliohusika katika kashfa za ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Ifike mahali swali hili lijibiwe: Kwa nini mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete hachukii uhalifu na watuhumiwa wa uhalifu? Nani anayetamani rais wa namna hii?
No comments:
Post a Comment