Friday, August 13, 2010

LIST OF SHAME

Orodha ya Mafisadi (List of Shame)






KANUNI/ VIGEZO VILIVYOTUMIKA





A. USHIRIKI WA MOJA KWA MOJA KATIKA VITENDO VYA UFISADI

Katika kundi hili wamo viongozi na/au maafisa wa umma na/au mawakala na/au washirika wao katika sekta binafsi ambao kwa namna mbali mbali wameshiriki katika kupora utajiri na/au fedha za umma na hivyo kulisababishia taifa na umma wa Watanzania ufukara na/au umaskini mkubwa.



B. USHIRIKI KATIKA KUTOA MAAMUZI YA KIFISADI

Katika kundi hili wamo viongozi wa umma ambao kwa kutumia nyadhifa na/au vyeo vyao katika utumishi wa umma wamefanya maamuzi ambayo kwayo taifa limepoteza mapato na/au utajiri na rasilmali zake na kuwaneemesha raia na/au taasisi za kiuchumi na/au za kibiashara za kigeni. Kwa mfano, viongozi wa umma walioshiriki katika kusaini mikataba mibovu katika sekta za madini na/au nishati na/au maeneo mengine yenye umuhimu mkubwa kwa maisha ya taifa na jamii ya Watanzania.
Orodha ya Mafisadi (List of Shame)






MISINGI YA KISHERIA/KISIASA YA ORODHA YA MAFISADI





A. KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 1977

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Sura ya 2 ya Sheria za Tanzania imeweka ‘Malengo Muhimu na Misingi ya Mwelekeo wa Shughuli za Serikali’ kuwa ni pamoja na mambo yafuatayo:[1]



Kwamba “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi….”;

Kwamba “lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi”; na

Kwamba “Serikali itawajibika kwa wananchi….”

….”

Katika kutekeleza malengo na misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali iliyotajwa, “… Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha:





Kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;

Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;

Kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja;







Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;

Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;

Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi;

….” [2]

Ibara ya 7(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeamuru kuwa “… Serikali, vyombo vyake vyote na watu wote na mamlaka yoyote yenye kutekeleza madaraka ya utawala, madaraka ya kutunga sheria au madaraka ya utoaji haki, watakuwa na jukumu na wajibu wa kuzingatia, kutia maanani na kutekeleza masharti yote ya Sehemu hii …” ya Katiba. Katiba pia imewapa viongozi wa umma “… wajibu wa kufuata na kuitii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano.”[3] Aidha, viongozi wa umma wamepewa “… wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi….”[4] Vile vile viongozi wote wa umma “watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi nay a pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”[5]



Licha ya masharti ya kikatiba yaliyotajwa hapo juu, viongozi wa umma waliotajwa katika Orodha hii ya Mafisadi walikuwa wanabanwa na masharti ya sheria nyingine za nchi yetu kama ifuatavyo:



B. SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA, 1995

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inamtaka Rais kuhakikisha kwamba taratibu zinatengenezwa zitakazojenga maadili na kuongeza imani ya wananchi kwa uadilifu wa viongozi wa umma na katika taratibu za utoaji maamuzi ndani ya Serikali na katika sekta ya umma. Katika kutekeleza wajibu wake, Rais anatakiwa kuweka taratibu thabiti za maadili katika utumishi wa umma ambazo:

Zitahakikisha kwamba kiongozi wa umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma;



Zitaweka taratibu za wazi za maadili kuhusu migongano ya maslahi kwa viongozi wa umma wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa;

Zitapunguza uwezekano wa migongano inayotokana na maslahi binafsi kuingiliana na shughuli za umma za viongozi wa umma na kuweka taratibu za utatuzi wa migongano hiyo inapotokea.

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma vile vile imeweka kanuni zinazotakiwa kuongoza utendaji wa viongozi wa umma:



kwamba wanapokuwa madarakani, viongozi wa umma watakuwa waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali;

kuhusiana na uwazi kwa wananchi, viongozi wa umma watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu;

kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma;

kuhusiana na maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya;

kuhusiana na maslahi ya umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma watapanga masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma;

kuhusiana na zawadi, viongozi wa umma hawatadai au kupokea manufaa ya kiuchumi zaidi ya zawadi ndogo ndogo, ukarimu wa jadi/takrima au manufaa mengine yenye thamani ishara, isipokuwa tu kama manufaa hayo yatatokana na mkataba au mali ya kiongozi wa umma;

kuhusiana na upendeleo, viongozi wa umma hawatatumia vyeo vyao rasmi katika kusaidia taasisi au watu binafsi katika mahusiano yao na serikali iwapo kufanya hivyo kutasababisha upendeleo kwa mtu yeyote;



Kuhusiana na mali ya serikali ambayo viongozi wa umma hawatatumia ama moja kwa moja ama kisiri siri, au kuruhusu kutumiwa kwa mali ya serikali ya aina yoyote, ikiwa ni pamoja na mali ya serikali iliyokodishwa kwa ajili ya kumnufaisha kiongozi wa umma;

Kuhusiana na ajira baada ya utumishi wa umma, viongozi wa umma hawatafanya vitendo vitakavyoshusha hadhi na heshima ya utumishi wa umma baada ya kuondoka katika utumishi ili kupunguza uwezekano wa matarajio ya ajira kuleta migongano ya maslahi kwa viongozi wa umma wanapokuwa katika utumishi wa umma; kupata upendeleo baada ya kuondoka katika utumishi wa umma; kutumia taarifa zinazopatikana kutokana na utumishi wa umma kwa maslahi binafsi; na kutumia utumishi wa umma kwa ajili ya kupatia nafasi za ajira nje ya utumishi wa umma.



--------------------------------------------------------------------------------



[1] - Ibara ya 8(1)

[2] - Ibara ya 9

[3] - Ibara ya 26(1)

[4] - Ibara ya 27(1)

[5] - Ibara ya 27(2)

No comments:

Post a Comment