Wagombea CCM Waanza Kumiminika Chadema!
Boniface Meena
BAADA ya kukosa ridhaa ya kugombdea ubunge kwa tiketi ya CCM kutyokana na chekeche la mwisho la halmashauri kuu ya chama hicho, waliokuwa wagombea ubunge na wanachama waandamizi watano wamekitema chama hicho na kuhamia Chadema.Baada ya kumalizika kwa kura za maoni ndani ya CCM ambazo ziliripotiwa kuwa zilijaa rafu, ukiukwaji wa taratibu na wagombea kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), tegemeo la mwisho la wagombea wote lilikuwa kwa halmashauri kuu ambayo ilimaliza kikao chake Jumamosi.
Chombo hicho chenye nguvu ndani ya CCM kilibatilisha ushindi wa wagombea watatu tu na kuidhinisha ushindi kwenye majimbo mengine yote licha ya kuwepo malalamiko na rufaa nyingi kupinga ushindi.
Naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe aliiambia Mwananchi kuwa wanachama wa CCM waliojiunga na chama chake kuwa ni Dk Raphael Chegeni, John Shibuda, Alatanga Nyagawa na Thomas Nyimbo.
Alisema kuwa kwa sasa tayari wameshawachukua hao na wanafanya jitihada za kumpata aliyekuwa mshindi kwenye kura za maoni jimbo la Nzega, Hussein Bashe ili aweze kugombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema. Bashe alimuangusha mbunge aliyemaliza muda wake, Lucas Selelii kwa kura nyingi, lakini CCM imemteua mshindi wa tatu kugombea ubunge.
Kabwe alisema kuwa tayari wameshampitisha Shibuda agombee ubunge wa jimbo la Maswa Mashariki kwa tiketi ya Chadema, huku Chegeni akipitishwa kugombea jimbo la Magu, Nyagawa jimbo la Njombe Kaskazini na Nyimbo jimbo la Njombe Magharibi.
"Hao wanne tayari tumeshakubaliana nao na tunazidi kuwatafuta wengine kama aliyeshindwa jimbo la Nkenge ambaye sitamtaja jina kwa sasa ila tuna matumaini ya kumpata pamoja na mwingine wa Shinyanga Mjini," alisema Kabwe.
Alisema kuhusu Bashe, Zitto alisema wanataka kumchukua ili kuwaonyesha Watanzania kuwa hawana ubaguzi wa rangi kwa CCM wanamjua Bashe kwa muda mrefu na inashangaza kwamba wakati huu ndio wamemgeuka kwa kigezo cha uraia.
"Tuko katika mazungumzo na Bashe tunajitahidi tumpate ili akasimame kwa niaba ya chama chetu huko Nzega... kwanza alipitishwa kwa kura nyingi ikimaanisha kuwa ataweze kukitetea chama ipasavyo," alisema Kabwe.
Alisema kuwa CCM si mamlaka ya kusema mtu fulani ni raia au si raia hivyo walichokifanya si sawa bali wameingilia mamlaka nyingine.
"Baba yake Bashe yuko Nzega pale, kwa nini wasiende kumfuata na kumuuliza? Hawa CCM wamekuwa na Bashe kwa muda mrefu iweje wanamgeuka sasa," alihoji Kabwe.
Aliongeza kusema: "Tunapinga ubaguzi kwa mtu yeyote, kwa hiyo tunamtaka."
Alipoulizwa kuhusu habari za kuhamia Chadema, Dk Chegeni alikiri kufanya mazungumzo na viongozi wa chama hicho lakini akawaeleza kuwa alikuwa safarini na alitarajia kumalizia mazungumzo, ingawa alisema mpaka jana jioni hakuwa amefikia uamuzi.
Alisema kuwa hawezi kuzugumzia kwa kina suala hilo kwa sasa kwa kwa sababu bado hajafanya uamuzi wa kujiunga na Chadema.
Kabla ya kujiunga na Chadema, Shibuda alikuwa katika ziara za kuaga wazee na marafiki zake wa siku nyingi ndani ya chama hicho tawala.
Shibuda, mwanasiasa mwenye historia nzito ndani ya CCM tangu enzi za Mwalimu, alifafanua kwamba asingeweza kufanya maamuzi magumu bila kuagana na wazee waliomlea katika chama.
Mbunge huyo wa zamani wa Maswa, alifafanua kwamba wapo wazee ndani ya CCM ambao anawaheshimu kwa kuwa ndio waliomtoa gizani na kumpandisha chati katika siasa.
Katika safari hiyo ya kuaga wazee, Shibuda alisema wiki iliyopita alikuwa visiwani Zanzibar alikokuita kuwa ndiko alikokulia na kukomaa kisiasa.
"Mimi niko Zanzibar nakutana na kuagana na wazee wangu. Nimelelewa Zanzibar ambako ndiko nilikokulia na kulelewa katika mazingira mazuri ya kisiasa," alifafanua.
Dk Chegeni, ambaye alikuwa mbunge wa Busega aliangushwa kwenye kura za maoni na Dk Titus Kamani Mlengenya, wakati Shibuda ambaye aliangushwa na Martine Makondo kwenye jimbo la Maswa Mashariki.
Naye Nyimbo alishinda kwenye kura za maoni lakini jina lake lilienguliwa na kupitishwa Gerson Lwenge na kwa upande wa Nyagawa atapambana na mwenyekiti wa CCM mkoani Iringa, De Sanga (Jah People) akiibeba Chadema.
Katika kura za maoni za CCM, zaidi ya wabunge 60, wakiwemo mawaziri watano, waliangushwa na halmashauri kuu haikuwa na huruma kwa mawaziri hao na wabunge wa muda mrefu, akiwemo mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani, John Malecela ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni za jimbo la Mtera.
Mbali na kigogo huyo ambaye alianza kuitumikia nchi tangu nchi ilipopata uhuru, wabunge wengine walioanguka ni Joseph Mungai (Mufindi Mashariki), Jackson Makweta (Njombe Kaskazini), Prof Philemon Sarungi (Rorya) na Dk Ibrahim Msabaha (Kibaha Mjini).
Wengine ambao wameshaanguka ni Bujiku Sakila (Kwimba), William Shelukindo (Bumburi), Raphael Mwalyosi (Ludewa) na Zainab Gama (Kibaha Mjini).
Wabunge wengine ambao hawajakitumikia chombo hicho kwa muda mrefu, lakini wameanguka kwenye kura za maoni ni Ludovic Mwananzila (Kalambo), Ponsian Nyami (Nkasi Kaskazini), Yono Kevela (Njombe Magharibi), Felix Mrema (Arusha Mjini), Ramadhan Maneno (Chalinze) na George Lubeleje (Mpwapwa).
Mawaziri walioshindwa vibaya kwenye kura za maoni ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Diodorus Kamala, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera (Korogwe Mjini) na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, James Wanyancha
No comments:
Post a Comment