Thursday, August 19, 2010

Wagombea CCM kupata upinzani mkali Arusha, Kilimanjaro




Paul Sarwatt, Arusha Agosti 18, 2010









BAADA ya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi za ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupenya tanuri la moto na chekeche la Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukabiliana na wagombea wa Upinzani katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 31 mwaka huu.



Changamoto hiyo kwa majimbo ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kama ilivyo kwa majimbo mengine nchini inatokana Upinzani kwa mara ya kwanza kusimamisha wagombea katika majimbo karibu yote.



NEC, chombo chenye nguvu ndani ya chama hicho

tawala kilimaliza vikao vyake mwishoni mwa wiki mjini Dodoma kikipitisha majina ya wagombea watakaokiwakilisha katika Uchaguzi Mkuu huku wengi wa waliopitishwa wakiwa ni wagombea walioongoza kura za maoni za Agosti Mosi.



Kura hizo za maoni zililamikiwa sana na wagombea karibu

wote na wengi waliyakatia rufaa matokeo wakidai kuwa kura hizo zilijaa rafu, ukiukwaji wa taratibu na wagombea kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za rushwa, na wengi walitarajia rufaa zao zingepatiwa majibu ndani ya NEC.



Wagombea waliopitishwa kwa majimbo ya Mkoa wa Arusha majimbo yao yakiwa katika mabano ni Dk. Batilda Burian (Arusha Mjini), Jeremiah Sumari (Arumeru Mashariki), Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi), Dk. Wilbald Slaa Lorri (Karatu), Michael Lekule Laizer (Longido), Edward Ngoyai Lowassa (Monduli) na Saning’o Kaika Ole Telele (Ngorongoro).



Waliopitishwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro ni Justin Salakana (Moshi Mjini), Dk. Cyril Agust Chami (Moshi Vijijini), Basil Pesambili Mramba (Rombo), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), David Mathayo David (Same Magharibi), Fuya Godwin Kimbita (Hai), Chrispin Theobald Meela (Vunjo), Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga) na Aggrey Mwanri

(Siha).



Manyara ni Kisyeri Werema Chambiri (Babati Mjini), Jitu Vrajil Soni (Babati Vijijini), Dk. Mary Michael Nagu (Hanang’), Benedict Ole Nangoro (Kiteto), Philip Sang’aka Marmo (Mbulu) na Christopher Ole Sendeka (Simnanjiro).



Dalili zinaonyesha kuwa wengi wa hawa waliopitishwa na NEC watakuwa na wakati mgumu katika kampeni kutokana na baadhi ya wagombea walioshindwa na wafuasi wao, kujiengua CCM na kujiunga na Upinzani na wengine kuwaunga mkono wagombea wa Upinzanikwa 'mbinu' tofauti.



Mkoani Arusha ambapo kuna majimbo sita ya uchaguzi kwa mara ya kwanza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kinaonekana kwa sasa kuwa chama cha Upinzani kilichojipanga vyema kitasimamisha wagombea katika majimbo yote yaani: Arusha Mjini, Monduli, Ngorongoro, Karatu, Longido, Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki.



Katika jimbo La Arusha Mjini mgombea wa CCM Dk. Batilda Burian ambaye alimwangusha Mbunge wa muda mrefu Felix Mrema katika kura za maoni, sasa atakuwa na mtihani mgumu dhidi ya mgombea wa CHADEMA Godbless Lema ambaye aligombea jimbo hilo mwaka 2005 wakati huo kwa tiketi ya chama cha Tanzania Labour (TLP).



Katika uchaguzi huo, Lema akiwa hafamiki kabisa kisiasa, alimpa wakati mgumu Mrema ambaye aliponea chupuchupu kushindwa na matokeo ya kura yalalamikiwa sana kuwa Lema alichezewa rafu na CCM katika dakika za mwisho wakati wa zoezi la majumuisho ya kura.



Aidha, katika jimbo hilo pia chama cha TLP kimemsimamisha Maxmilian Lyimo ambaye pia anatarajiwa kutoa changamoto ingawa mgombea huyo hafahamiki kwa wapiga kura wengi, huku Chama cha Wananchi (CUF) nacho kikitarajiwa kusimamisha mgombea.



Katika Jimbo hilo la Arusha Mjini wagombea wanaopewa nafasi ni Dk. Burian na Lema lakini matokeo ya mwisho yatategemea uendeshaji wa kampeni na maamuzi ya mwisho ya wapiga kura wa Arusha. Tayari Lema amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.



Katika jimbo la Karatu ambalo ni ngome ya CHADEMA kwa miaka 15 sasa, DK.Wilbard Slaa Lorri ambaye amepitishwa na CCM anapambana na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Israel Yohana Nat’se ambaye amepitishwa na CHADEMA kupeperusha bedera ya chama hicho.



Mchungaji huyo ameingia katika kinyang’anyiro hicho kujaribu kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Wilbroad Peter Slaa ambaye baada ya kuwatumikia wananchi wa Karatu kwa miaka 15 ameteuliwa kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.



Bado haijafahamika iwapo vyama vingine vitasimamisha wagombea katika jimbo hilo, lakini hata kama wataingia wengine, bado ushindani utabaki kuwa kati ya CCM na CHADEMA ambavyo vimetawala siasa za jimbo hilo tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.



Wachunguzi wa mambo wanaeleza kuwa, hata hivyo, itakuwa kazi ngumu kwa CCM kushinda jimbo hilo kutokana na kukubalika sana kwa mgombea wa CHADEMA ambaye anaelezwa kuwa karibu na wananchi wengi kutokana na kuwahi kuwa mratibu wa miradi ya maendeleo ya jamii ya Kanisa, kazi ambayo imemfanya kufahamika kwa wapiga kura wengi tofauti na mgombea wa CCM.



Lakini maoni hayo yasiyoipa CCM nafasi, yanapuuzwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Karatu, John Tipe, aliyekaririwa na gazeti moja la kila siku akijigamba kuwa muhula wa mwisho CHADEMA kutawala Karatu ulikuwa huu unaoishia mwaka 2010 na CCM ilikuwa imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha kuwa kinaibuka na ushindi.



Jimbo la Monduli ambalo Mbunge wake wa muda mrefu Edward Lowassa hakuwahi kupingwa tangu uchaguzi wa mwaka 1995 pia limepata mgombea kutoka CHADEMA ambaye ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Assemblies of God, Amani Ole Siranga Mollel.



Mchungaji huyo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Building East Africa Community Network,

inayojishughulisha na masuala ya amani, alichukua fomu Jumatatu kuwania nafasi hiyo akisindikizwa na umati wa wananchi wa Monduli.



“Tayari nimechukua fomu ya kushiriki uchaguzi kupitia CHADEMA na lengo langu ni kuleta mabadiliko ya kweli jimboni… Wananchi wengi hapa wamenieleza kuwa hawakuwa na mbadala ndiyo maana walikuwa wanalazimika kumpigia kura mgombea mmoja tu,” alisema mchungaji huyo katika mazungumzo ya simu na Raia Mwema kutoka Monduli.



Ingawa Mchungaji huyo anajipa matumaini ya kumwangusha Lowassa, itamlazimu afanye kazi ya ziada kufikia lengo hilo kutokana na historia ya Lowassa katika siasa za jimbo hilo na Taifa kwa ujumla na kazi kubwa ambayo amefanya ya kusimamia miradi ya maendeleo katika jimbo hilo kwa kiwango cha juu iliyomjengea imani miongoni mwa wapiga kura.



Katika Jimbo la Ngorongoro, mbunge aliyemaliza muda wake Saning’o ole Telele wa CCM anatarajiwa kupambana na mgombea wa CHADEMA, Lazaro Moringe ole Parkpuny ambaye amepata kuwa mbunge wa jimbo hilo katika miaka ya 1990 akiwakilisha CCM.



Parkpuny alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 1995 na William Ole Ntiman na tangu wakati huo hakusikika tena katika siasa za wilaya hiyo hadi alipoibukia CHADEMA mwaka huu, yuko katika majaribu makubwa ya kushinda kutokana na historia ya jimbo hilo linalokaliwa na idadi kubwa ya wafugaji wa Kimasai.



Ni vigumu kwa Upinzani kushinda uchaguzi katika maeneo kama hayo kutokana na elimu duni ya masuala ya uraia kwa jamii za wafugaji lakini pia kigezo kikubwa huwa ni uaminifu wa wapiga kura kwa kiongozi aliyeko madarakani na mazingira hayo yanampa telele nafasi kubwa ya kushinda.



Jimboni Longido, kwa mara ya kwanza mbunge aliyepita, Lekule Michael Laizer amepata mpinzani ambaye ni Bi. Paulina Lukas Laizer anayegombea pia kwa tiketi ya CHADEMA.



Bi Paulina ni kati ya wagombea waliovunwa na CHADEMA kutoka CCM kutokana na migogoro ya kura za maoni iliyosababisha ashindwe katika kugombea nafasi za udiwani kupitia Viti Maalumu na hivyo kuchukua uamuzi wa kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.



Yote kwa yote Bi Paulina hapewi nafasi kubwa ya kumshinda Lekule kutokana na mfumo dume uliotapakaa katika jamii ya wafugaji ambao hautoi fursa kwa jamii kuongozwa na viongozi wanawake.



Katika jimbo la Arumeru Magharibi Gooluck Medeye wa CCM atapambana na Mathias ole Kisambo wa CHADEMA ambaye ni mfanyabiashara na mkulima maarufu mjini Arusha.



Ahueni ya Kisambo ni kuwa migogoro iliyotokana na kura za maoni zilizomwezesha Medeye kuwaangusha mbunge aliyepita, Elisa Mollel, na Mkuu wa Wilaya Songea, Loi Thomas Sabaya bado inatokota.



Mollel na Sabaya bado wana nguvu na ufuasi mkubwa jimboni hata kama wameshindwa na Medeye, ikitokea wafuasi wakaamua kutompigia kura Medeye, wakampa kura hizo Kisambo, patakuwa na patashika.



Katika jimbo La Arumeru Mashariki, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari atapambana na mwanasiasa “chipukizi” Joshua Nasari ambaye amehitimu masomo ya fani ya Sosholojia na Utawala mwaka 2009 katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Mgombea huyo ni zao la mpango uliaonzishwa na CHADEMA wa kuwashawishi wanafunzi wa elimu ya juu kujiunga na chama hicho.



Mkoani Kilimanjar, katibu wa CHADEMA mkoani humo, Basil Lema hakupatikana kuelezea mikakati ya chama chake lakini jimbo ambalo macho na masikio ya wengi yatakuwa yamelekezwa ni jimbo la Moshi mjini ambapo Mbunge wake,

Philemon Ndesamburo atapambana na Justin Salakana aliyepitishwa na CCM.



Katika jimbo hilo hata hivyo bado Ndesamburo ambaye ni maarufu mjini Moshi kwa jina la “ndesa pesa” ataibuka mshindi kutokana na uzoefu wake katika siasa za mkoa wa Kilimanjaro na pia zaidi mgawanyiko wa muda mrefu katika chama cha CCM kutokana na sababu mbalimbali lakini

hasa matokeo ya kura za maoni.



Jimbo lingine mkoani humo ni Jimbo la Vunjo ambako CCM wamempitisha mwanasheria Crispin Meela anayetarajiwa kupambana na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo miaka ya nyuma

na baadaye kugombea ubunge mara tatu bila mafanikio.



Ingawa Mrema kitaifa amepoteza mvuto wa kisiasa kutokana na kauli zake tata katika masuala mbalimbali, inaaminika kuwa bado ana wafuasi wengi katika jimbo hilo ambalo yeye huliita “uwanja wa nyumbani” na pia kuna madai ambayo hata hivyo hajathibitishwa kuwa kuna mpango wa

siri baina yake na baadhi ya viongozi wa CCM ambao watamsadia ashinde huku na yeye akiwaangamiza viongozi wengine wa upinzani kwa 'kulipua mabomu' yao.



Jimbo la Hai pia litakuwa katika hekaheka baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA kutanga nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo na habari hizo zitakuwa si njema sana kwa mbunge aliyemaliza muda wake, Fuya Kimbita ambaye pia ameptishwa na CCM kuwania nafasi hiyo tena.



Mbowe alishawahi kuwa Mbunge wa Hai kati ya mwaka 2000-2005 alipokwenda kugombea nafasi ya Urais ambapo alishindwa na Jakaya Kikwete wa CCM lakini sasa akioongoza CHADEMA na kukipatia umaarufu na nguvu ya kisiasa nchini amerudi kugombea nafasi ya Ubunge na anapewa nafasi

kubwa kutokana kukubalika kwake na wananchi lakini pia kutokana na kuwa na nguvu ya ukwasi wake.



Majimbo mengine ya Mwanga, Rombo, Same Magharibi, Same Mashariki na Moshi Vijijini na Siha bado wagombea wa upinzani watakaosimama walikuwa hawajafahamika kutokana na CHADEMA kuchelewesha kutoa orodha ya

mwisho ya wagombea wake lakini kutokana na mkoa wa Kilimanjaro kihistoria kuwa chimbuko la upinzani, basi lolote linaweza kutokea.



Mkoani Manyara, majimbo ya mkoa huo ambayo hayapewi nafasi kwa wapinzani kufanya vizuri ni Simanjiro na Kiteto ambayo wagombea wake kupitia CCM, Christopher ole Sendeka na Benedict Nangoro wanaweza kushinda kwa

urahisi kutokana majimbo hayo kukaliwa na wafugaji wengi wa Kimasai ambao bado ni 'waamininifu' kwa chama tawala cha CCM.



Lakini moja majimbo ambayo yatakuwa katika pilikapilika kubwa ni jimbo la Mbulu ambalo Mbunge wake anayetaka kuweka rekodi ya kuwa bungeni kwa miaka 30, Philip Marmo atakuwa katika mtihani mgumu wa kupambana na mgombea wa CHADEMA, Boay Mustafa Akonaay ambaye ni Katibu

Mkuu wa Chama cha Wakala wa Utalii Nchini (TATO) na pia ni mwanasheria wa kujitegemea.



Marmo alianza kuwa Mbunge wa Mbulu tangu mwaka 1985 hadi sasa lakini alinusurika kung’olewa na Akonaay katika uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo alishinda kwa tofauti ya kura zisizozidi 2,500 na tayari katika uchaguzi wa mwaka huu kampeni kali zinatarajiwa hasa baada ya Marmo

kuponea chupuchupu kuangushwa katika kura za maoni na Michael Lorri ambaye ni Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro.



Aidha katika jimbo la Haang’ pia Dk. Mary Nagu anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa hasimu wake kisiasa aliyemshinda katika kura za maoni, Rose Kamili ambaye sasa ameamua kuhamia CHADEMA na matokeo ya mwisho katika jimbo hilo yatategemea zaidi uendeshaji wa kampeni.



Katika majimbo mawili ya Babati Vijijini na Babati Mjini wagombea wa upinzani walikuwa bado hawajafahamika lakini pia chochote kinaweza kutokea katika majimbo hayo iwapo tu watatokea wagombea wa upinzani wanaokubalika kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment