Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kujitwalia majimbo ya ubunge kabla ya upigajikura hapo Oktoba 31 mwaka huu, baada ya idadi ya wagombea wake wakiwemo mawaziri kupita kwa ushindi wa 'mezani' wa mapingamizi dhidi ya washindani wao na kuwezesha chama hicho, kuweka kibindoni majimbo 16 hadi sasa hivi.
Hadi jana, CCM iliweza kujitwalia majimbo zaidi likiwemo Mlele kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baada ya mgombea wa CUF Abasi Rashid, kujitoa kwenye mbio hizo huku katikia Jimbo la Mtama, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akipita kwa mlango huo wa pingamizi dhidi ya Isaya Ndaka wa TLP, baada ya kukosa idadi ya wadhamini wanaohitajika.
Kasi hiyo ya CCM ilizidi kuongezeka jana baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha kupita kwa mlango huo wa pingamizi dhidi ya mshindani wake kutoka Chadema Wenje Ezekie huku Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, naye akipeta.
Hadi sasa wana CCM waliotangazwa kuteuliwa wabunge na majimbo yao kwenye mabano ni Pinda (Mlele ), Mohamed Dewiji (Singida mjini), January Makamba (Bumbuli), Job Ndugai (Kongwa), Deo Filikunjombe (Ludewa), Gregory Teu (Mpwapwa), Anne Makinda (Njombe Kusini), William Lukuvi (Isimani, na Celina Kombani ( Ulanga Mashariki).
Wengine ni Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba kusini), Profesa David Mwakyusa (Rungwe Magharibi), Philip Mulungu (Songwe) na (Mtama, kwa Membe).
Jimboni Nyamagana, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo alikubaliana na pingamizi la Waziri Masha dhidi ya mshindani wake ambaye baadhi ya taarifa ikiwemo uraia wake, zilikuwa tata.
Akitoa uamuzi wa tume ya uchaguzi jimbo la Mwanza chini ya msimamizi Willison Kabwe alisema, Wenje ameenguliwa katika mbio hizo kutokana na kukosa sifa ya uraia ikiwa ni pamoja na kudanganya makazi.
“Pingamizi alilowekewa Wenje, alidaiwa kuwa siyo raia, katika utetezi wake hakuweza kuwasilisha ushahidi wowote kuonyesha uraia wake kama vile vyeti vya kuzaliwa, kuhitimu shule na alizosomea hapa nchini," alifafanua na kuongeza:,
"Hakuweza kuwasilisha paspoti wala kiapo chochote na shahada ya kupigia kura, basi nakubaliana na pingamizi la kuwa siyo raia.”
Ingawa Masha aliweka pingamizi hilo kama mgombea ubunge, lakini kisheria wizara anayoongoza ndiyo yenye dhamana ya uraia wa wageni na wazawa, kwani akiwa waziri anaweza kumtangaza nani ni raia na nani si raia.
Katika pingamizi la pili dhidi ya Wenje, Masha alidai alidanganya nafasi yake ya kazi kuwa yeye ni mtumishi wa cheo cha ‘Country Manager’ wa kampuni ya Nation Media Group, wakati yeye ni mtumishi wa cheo cha Sales Manager (Meneja Mauzo).
Mtoa pingamizi (Masha) aliweka pingamizi hilo na kuonyesha ushahidi wa barua, kutoka kampuni hiyo ikipinga maelezo ya mgombea huyo.
“Katika utetezi wake Wenje aliwasilisha Job description na alikana kumtambua mmoja wa viongozi wa juu, akisema hahusiki na kampuni hiyo ya Nation Media group," aliweka bayana Kabwe na kuongeza:,
"Nilitegemea Wenje angewasilisha barua ya ajira kutoka kwa mwajiri wake ikithibitisha cheo chake alichodai ana kitambulisho chake. Hivyo nakubaliana na pingamizi kuwa alidanganya nafasi yake ya kazi.”
Hoja nyingine katika pingamizi hilo iliyomtupa mgombea huyo nje ya mbio za kuwania jimbo hilo, inahusu tamko la wadhamini katika fomu na 8 C, ambayo alichanganya tarehe ya uteuzi akidai utafanyika Oktoba 31 mwaka huu badala ya Agosti 19 mwaka huu, jambo ambalo alipaswa kuwa makini nalo kutokana na kugombea nafasi hiyo nyeti.
Pingamizi la mwisho ambalo aliwekewa lilikuwa ni eneo lake la makazi, Wenje alieleza anakaa mtaa wa Bulola ‘A’ jijini Mwanza, jambo ambalo siyo kweli.
“Katika maelezo yake alieleza anamiliki nyumba namba BSL/BLL/01/219 mtaa huo. Alipaswa kuwasilisha nyaraka za uthibitisho wa umiliki wa nyumba aliyotaja kumiliki kutokana na kukosekana kwa uthibitisho huo mimi msimamizi wa uchaguzi nakuwa na shaka na ukazi wake,” alizidi kupigilia msumari Kabwe.
Alisisitiza kwamba, kwa kuzingatia sababu zilizobainishwa hapo juu, "nakubaliana na sababu za pingamizi hivyo kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 pamoja na marekebisho yake natamka rasmi kutengua uteuzi wa bwana Wenje."
Kutokana na maamuzi hayo ya msimamizi wa uchaguzi, Masha anabaki kuwa mgombea pekee wa ubunge katika jimbo hilo la Nyamagana.
Hata hivyo, akizumgumza uamuzi huo Wanje alisema aliupokea na kuongeza kwamba, kwa sasa anawasiliana na viongozi wa chama cheke mkoa na kisha atasafiri kuelekea Dar es Salaam makao makuu ya chama ambako atakutana na wanasheria wa Chadema kuona namna ambayo watakata rufaa kupinga uamuzi huo wa msimamizi wa uchaguzi.
“Sikubaliani na umuzi huo na lazima tutakata rufaa, ikishindikana rufaa hiyo basi nitakwenda wilayani Rorya mkoani Mara kufanya mkutano mkubwa kuwaeleza wananchi wanaonitambua kuwa mimi ni mzaliwa wa Rorya wajue Waziri wa Mambo ya ndani ameninyang’anya uraia,” alitangaza azma hiyo.
Aliweka bayana kwamba, katika mkutano wake kwa wananchi wa Rorya atawaeleza wagome kulipa kodi kwa serikali ya Tanzania kwa vile Rorya siyo eneo la Tanzania na wao licha ya kuzaliwa hapo siyo raia.
SENGEREMA, wagombea wawili kutoka vyama vya upinzani waliokuwa wanashiriki mbio za kuwania nafasi ya ubunge wilayani Sengerema, wametupwa nje kutokana na kukosa sifa za kugombea.
Wagombea hao kutoka CUF, Mbaraka Sadi Chilu pamoja na mgombea wa Chadema, wameenguliwa katika dakika za mwisho baada ya kushindwa kujitetea kutokana na makosa ambayo yamejitokeza.
Akizungumza kwa njia ya simu Msimamizi wa Uchaguzi Wilayani hapo Erica Msika, alifafanua kwamba mgombea wa CUF alishindwa kusaini fomu namba 10 pamoja na kutokuheshimu maadili ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo, kutokana na makosa hayo ni dhahiri mgombea huyo amekosa sifa ya kuwa mgombea halali kupitia tiketi ya chama chake .
Kuhusu mgombea wa Chadema, Magafu Salvatori, msimamizi wa uchaguzi alisema uteuzi wake ulitenguliwa baada ya wadhamini wake kukosa sifa ya kumdhamini.
Aliweka bayana kwamba, kuna baadhi ya wadhamini wake vitambulisho vyao vya kupigia kura vilikuwa havijasajiliwa katika daftari la mpigakura, kosa ambalo linawapotezea sifa ya kuwa wadhamini wa mgombea.
Msimamizi huyo aliongeza kwamba, pamoja na wadhamini hao kukosa sifa mgombe huyo hakusaini fomu ya tamko na kushindwa kujitetea sababu zilizomfanya ashindwe kuzisaini.
Msika alisisitiza kwamba, baada ya kupitia pingamizi hilo kutoka kwa muweka pingamizi (Ngeleja), alibaki kuwa mgombe pekee kwa tiketi ya CCM katika Jimbo hilo.
Wakati huo huo, pingamizi zote ambazo zilifikishwa kwa msimamizi wa uchaguzi kutoka katika Jimbo la Ukerewe, zimetupiliwa mbali.
Katika mapingamizi hayo mwanasiasa wa mkongwe, Getrude Mongella, alimwekea pingamizi mgombea wa Chadema, Salvatory Machemli, kwa madai alikiuka kanuni za uchaguzi huku naye akiwekewa pingamizi na mgombea huyo wa upinzani kwa madai ya (Mongella), alikosea kujaza kazi yake.
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Dk Leonard Masale, alisema baada ya kupitia mapingamizi yote na kupitia vielelezo vyote aliamua kuyatupilia mbali hivyo wagombea wote watabaki katika mbio hizo kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba 31.
SINGIDA, mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Singida Mjini, Mohammed Dewji, naye amepata ushindi huo wa mezani baada ya wapinzani wake watatu kuenguliwa kutokana na fomu zao kuwa na mapungufu mengi.
Waliokuwa wapinzani wa Dewji ni makamu mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP) Omari Sombi, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Siuyu, Josephat Isango kupitia Chadema na Rashid Mindika wa CUF.
Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Yona Maki, alifafanua kwamba, wagombea wote watatu walioenguliwa, walielezwa siku wanachukua fomu hizo kwamba watapaswa kuzijaza na kuzirudisha siku tatu kabla ya siku ya mwisho kisheria ili zikaguliwe na endapo zitakuwa na mapungufu, wazirekebishe kabla ya muda kumalizika.
"Ndugu zangu hawa hawakufanya hivyo na walipozirejesha na kukaguliwa, zilikutwa na mapungufu mengi na muda wa wao kuzirekebisha, ulikuwa hautoshi na ndio maana ulipofika muda wa kufunga pazia kwa zoezi hilo, wenyewe wakawa hawajakamilisha shughuli hiyo ya kuondoa mapungufu," aliweka bayana.
Akimzungumzia Dewji ambaye ametangazwa rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo la Singida mjini, msimamizi huyo alisema alirejesha fomu zake siku tatu kabla ya muda kwisha na fomu zake zilikaguliwa na kukutwa hazina tatizo.
Maki aliongeza kwamba, kwa sasa zoezi la kumtafuta mbunge wa Jimbo la Singida mjini limekamilika na wamebakia na zoezi la madiwani.
Naye Dewji kwa upande wake alisema hana la kuzungumza zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uweza wake, na kwamba alimsaidia kuwaumbua wale ambao walikuwa hawamtakii mema kwa kumzushia mapingamizi yasiyokuwa na msingi, fitina, majungu na kueneza taarifa zenye lengo la kumpaka matope.
Habari hii imeandikwa na Frederick Katunlanda, Mwanza, Sheilla Sezzy, Sengerema, Gasper Andrew, Singida
No comments:
Post a Comment