Tuesday, August 10, 2010

JK HATAKI KURA ZA WAFANYAKAZI

Watu Wazima Ovyoo: CCM Wakanusha JK Hajakataa Kura za Wafanyakazi


Miongoni mwa mambo yanayoipa kiburi CCM ni imani ilishamiri miongoni mwa viongozi wa chama hicho kuwa Watanzania hawana kumbukumbu,hawajui kutofautisha zuri na baya,wavumulivu kupita kiasi,na ni viumbe wa kupelekeshwa tu.Yayumkinika kuhitimisha kwamba imani hiyo ya viongozi hao inasababishwa na mambo makuu mawili:Kwanza,dharau,kiburi,ubinafsi,na kubwa zaidi ya yote,ufisadi.Sababu ya pili,ni namna Watanzania wengi wanavyoendelea kukiamini chama ambacho kilishawatelekeza miaka kadhaa iliyopita.



Katika sababu hii ya pili,mfano mzuri ni ule wa mume anayemnyanyasa mke kupindukia lakini mapenzi ya mke huyo yanazidi kudumu akitarajia mumewe atapatwa na akili au huruma.Kwa bahati mbaya,utiifu huo wa mke kwa mume mnyanyasaji huishia kutafsiriwa na mume huyo kuwa mkewe “amenasa kwenye zege”,hana ujanja wa kuomba talaka au kukabiliana na manyanyaso ya mume huyo.



Ni katika mantiki hiyo ndipo leo tunasikia kioja cha mwaka ambapo “msema chochote” wa CCM,Tambwe Hizza (ambaye bado anaugulia maumivu ya kubwagwa kwenye kura za maoni huko Temeke) akikurupuka na kudai Rais Jakaya Kikwete hajawahi kutamka kuwa “hataki kura za wafanyakazi”.



Huyu Tambwe ni mhuni,hana nidhamu kwa Watanzania (kama alivyokuwa mhuni kwa kuapa kumtukana mama yake mzazi),na anafikiri bado tunaishi katika zama zile ambapo kama mwananchi hakuhudhuria mkutano uliohutubiwa na kiongozi husika,basi tegemeo pekee ni magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo au “midomo ya serikali” yaani Radio Tanzania na Daily News.Na vyombo vyote hivyo vya habari vilikuwa na unyenyekevu wa kuchefua kwa namna vilivyokuwa vikifanya kila liwezekanalo kupendezesha hotuba au kauli za watawala wa enzi hizo.



Japo vyombo vya habari vya serikali (Habari Leo,Daily News na TBC) bado vimeendelea kukumbatia siasa za chama kimoja kwa kuipendelea CCM waziwazi na kupuuza kuwa vinaendeshwa kwa fedha za walipakodi (ambao takriban milioni 35 kati yao sio wanachama wa CCM) lakini angalau siku hizi tuna vyombo binafsi vya habari pamoja na social media (blogs,youtube,facebook,twitter,nk) na hiyo inasaidia kwa kiasi kikubwa “kutofautisha mchele na pumba”.



Lakini kutokana na dharau zao na kutojali,Tambwe na CCM wanajifanya hawajui kuwa hotuba ya Kikwete kuhusu tishio la mgomo wa wafanyakazi ipo mtandaoni.Mtandaoni kuna video zenye hotuba hiyo,na uzuri wa mtandao ni kwamba unahifadhi kumbukumbu vyema sana.Kwahiyo hata kama CCM wangetaka “kufuta maneno hayo ya JK” bado wangekabiliwa na kigingi katika kufuta kumbukumbu zilizozagaa mtandaoni.Pengine wanafahamu sana kuhusu hilo lakini wanajipa matumaini kwa kuamini kuwa “Watanzania ni wanyonge sana na hawaweza kusaka kumbukumbu za kauli hiyo ya Kikwete”.Au pengine ni jeuri tu ya madaraka na imani kwamba kiongozi ana ruhusa ya kuahidi chochote,kusema lolote na kufanya chochote na asihukumiwe na umma.



Leo Tambwe anasema Kikwete hajawahi kutamka kuwa hahitaji kura za wafanyakazi.Je atakanusha pia kuwa Kikwete hajawahi kusema mimba za wanafunzi wa kike ni kiherehere chao?Au hakuwahi kutamka kuwa hajui kwanini Tanzania ni masikini?Au hajawahi kutamka kuwa anawafahamu wala rushwa lakini anawapa muda wa kujirekebisha?Au hakuwahi kuahidi kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana?Au Tambwe pia atakabusha kuwa Kikwete hakutumia mfano wa MBAYUWAYU?



Kwani Tambwe au CCM,au hata JK mwenyewe,hawakukanusha habari zilizoandikwa na gazeti la Mwananchi chapisho la mtandaoni Mei 3, 2010 na kupewa kichwa cha habari "JK: Nipo Tayari Kukosa Kura Zenu" na kumnukuu "(Kikwete) alifafanua kuwa kima cha chini cha mshahara cha Sh315,000 kwa mwezi kinachopigiwa debe na Tucta, serikali haiwezi kukitekeleza na kama hilo ni shinikizo kwake ili wafanyakazi wampatie kura kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, hahitaji kura zao". (BONYEZA HAPA KUSOMA HABARI HIYO)



Ni dhahiri hili zoezi la kukanusha kauli halitafanikiwa.Liliwezekana katika zama ambapo Watanzania uhuru na access ya habari ilikuwa kwa ridhaa ya watawala lakini sio sasa ambapo blogs,webforums,facebook,twitter,youtube,nk zinapatikana kila kona ya dunia alimradi kuna internet connection.



Dharau na jeuri ya CCM iliwafanya wajisahau kwenye usingizi wa pono huku JK akitoa baadhi ya kauli zisizotarajiwa kutoka kwa mwanasiasa anayetarajia kuomba tena ridhaa ya wananchi kuwaongoza tena.Wakati huo walikuwa na uhakika wa asilimia zaidi ya 100 kuwa JK na CCM yake kurejea madarakani ni suala la muda tu na sio “if watarejea”.Lakini ghafla,baada ya Chadema kumtangaza Dkt Wilbroad Slaa kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais,CCM wametahayari.Hawakuona umuhimu wa kukanusha kauli hiyo ya JK mpaka baada ya kumsikia Dkt Slaa akiwaeleza wafanyakazi kuwa “anahitaji kura ambazo Kikwete hazihitaji”.Ghafla,CCM wanakugundua kuwa kauli hiyo haikuwa mwafaka,lakini kwa dharau zao badala ya kuomba radhi au kutafuta suluhu wanakimbilia kukanusha.



Nimeandika makala kadhaa katika blogu yangu kuhusu umuhimu wa CCM kuwaomba radhi Watanzania kwa madudu mbalimbali waliyotufanyia badala ya wao kuendelea kujigamba kuhusu “mafanikio yaliyopatikana katika utawala wao”.Yani wanataka kutuambia kuwa hata kushamiri kwa ufisadi ni mafanikio?Kwanini wasingetumia busara ya kutueleza “mafanikio” yao kisha wakaonyesha uungwana kwa kueleza maeneo ambayo kimsingi “wametuangusha”?Hawawezi kufanya hivyo kwa vile wanatudharau,wanatuona wajinga tusiojua kutenganisha mema na mabaya,wasahaulifu tusiokumbuka hata mahitaji yetu muhimu.



Tayari chama hicho tawala kimeshaonyesha “mchecheto” kwa kukacha kushiriki mdahalo wa wagombea urais kabla ya “kulialia” kuwa Chadema inacheza rafu “kwa kuanza kampeni kabla ya muda wake”.Ukichanganya na songombingo linaloendelea ndani ya chama hicho katika mchakato wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao ni dhahiri kuwa kwa mara ya kwanza CCM inaanza kuona dalili za kung’olewa madarakani.Na huenda moto mkubwa zaidi ukawaka ndani ya chama hicho baada ya mchujo wa wagombea baadaye mwezi huu.



Tahayari iliyowakumba CCM inaweza kuwa silaha nzuri kwa Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla.Kwa kauli kama hizi za akina Tambwe,ni rahisi kwa Chadema kuwaonyesha Watanzania namna gani chama hicho kinavyowadharau.Ndio!Kwani kama si dharau ni nini basi pale mtu anapokutukana halafu baada ya kitambo akaibuka na kukanusha kuwa hajakutukana japo ushahidi upo bayana?CCM inajikaanga kwa mafuta yake yenyewe.Dharau na jeuri yao inaweza kuwa mtaji mzuri wa anguko lake.



Kwa wale wote wenye uchungu wa dhati kwa nchi yetu na waliochoka kufisadiwa na CCM,kitendo cha chama hicho kukanusha kuwa JK hajawahi kukataa kura za wafanyakazi kinapaswa kutafsiriwa kama namna Watanzania “watakavyoingizwa mkenge tena kama mwaka 2005” ambapo chama hicho kiliahidi mambo chungu mbovu lakini badala yake matokeo ni kushamiri kwa ufisadi.Kama mwenyekiti wa chama hicho anaweza kutoa kauli hadharani kisha chama chake kikaibuka kudai kuwa hajatoa kauli hiyo,je kwanini tusiamini kuwa mgombea urais wa chama hicho (JK) ataishia kupuuza ahadi anazotoa sasa na wakati wa kampeni,na CCM ikiulizwa ikaishia kukanusha kuwa hajwahi kuahidi hivyo?



Watanzania sasa tumepatiwa nafasi adimu ya kuondokana na CCM.Katika chaguzi zilizotangulia tulikuwa hatuna uhakika na wagombea waliosimamishwa kuchuana na mgombea wa CCM lakini safari hii tumebahatika kupata mtu ambaye rekodi yake inajidhihirisha bayana.Na kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya chaguzi nchini mwetu ambapo CCM inaonekana ikianza kutahayari waziwazi baada ya mwamko ulioletwa na Chadema na Dkt Slaa,huo ni uthibitisho tosha kuwa mafisadi wamegundua kuwa siku zao zinahesabika.



Tusirejee makosa ya huko nyuma ya kujaa kwenye mikutano lakini kura zinakwenda CCM.Safari hii,acha watoe rushwa zao (na mzipokee tu kwa vile ni fedha walizowafisadi) lakini kura ziende kwa Dkt Slaa.Dawa ya kung’oa ufisadi ni kung’oa mmea unaolea ufisadi,na mmea huo ni CCM.



Watu Wazima Ovyoo: CCM Wakanusha JK Hakukataa Kura za Wafanyakazi
KULIKONI UGHAIBUNI

No comments:

Post a Comment