No mdahalo no vote
Hakuna mpambe wala pamba bali mapambano ya hoja na sera badala ya sura Vijana Bwana. Sijui wakoje siku hizi. Wakati sisi tulikuwa tayari kukubali tunayoambiwa, tuliwaamini watu, vijana wa siku hizi wanataka kuhoji kila kitu. Wanataka kupima na kujiamulia wenyewe. Hebu angalia pepe hili hapo chini. Mwishiwa Makengeza, Shikamoo! Na baada ya kushika miguu yako bila sababu (hivi kweli hatuwezi kupata salaam nyingine ya heshima?) naomba nitoe dukuduku zangu kwako kama kijana wa nchi yetu. Sisi vijana ndio walio wengi katika nchi hii, tena walio wengi sana, lakini inavyoonekana, watu wanataka tushike miguu yao tu, badala ya kuelewa na kutenda kwa faida ya nchi. Kwa kuwa wametuona tumeinama tu wanatudharau, na tukiasi kuinama wanatuita wahuni wasio na heshima blaa blaa blaa hadi balaa.
Ngoja nijieleze kidogo. Kwanza nakuandikia wewe kwa sababu naamini unataka mabadiliko chanya kwa ajili ya taifa letu. Si kwa sababu ya chama hiki au kile, bali uchaguzi huu unatoa fursa nzuri kuachana na miaka hii mitano ya kashfa baada ya kashfa. Unatoa fursa kwa ajili ya kupeleka kizazi kipya (si kiumri, kimtazamo) bungeni ili, wawe wa chama hiki au kile, waweze kuweka misimamo na sera bora zaidi. Lakini ili kufanya hivyo, tunahitaji kuwasikia wagombea mbalimbali wakibadilishana mawazo, wakipeana changamoto, kukosoana na kurekebishana, siyo tu kutamba jukwaani, bali kukutana pamoja ili tuweze kupima nani anasema ukweli zaidi, nani ana sera zaidi, nani amefikiria kwa kina zaidi kwa ajili kututoa katika lindi la kukata tamaa linalowameza vijana wengi. Ndiyo. Huwezi kumpima mtu jukwaani maana anatamba peke yake na wapambe wanampamba akitamba (na kumjaza pamba masikioni).
Tunataka kumsikia akikabiliwa na changamoto kutoka kwa mwingine, asiyekubaliana na mtazamo wake, au sera zake, au takwimu zake. Kwa kiasi fulani kazi hii inaweza kufanywa na vyombo vya habari lakini mpaka sasa sijaona uchambuzi wowote wa sera za vyama mbalimbali, tofauti zao, na kadhalika. Sijawaona wakihoji au kuchambua takwimu zinazotolewa na upande wowote. Lakini zaidi ya yote tunataka kupima na kuamua mwenyewe kwa kuwasikiliza laivu. Hapa hakuna mpambe wala pamba bali mapambano ya hoja na sera badala ya sura. Ndiyo maana vijana tunasema
NO MDAHALO NO VOTE
Kwa maana kwamba asiyekubali kushiriki mdahalo ili kutuwezesha kupima na kuamua tumchague nani kwa faida ya taifa hawezi kupata kura yetu. Na tunasisitiza mdahalo utangazwe na wagombea wote wakaribishwe kushiriki. Asiyekubali atawakilishwa na kiti kitupu na wengine watapewa nafasi ya kujieleza bila upinzani kutoka kwa yule au wale waliokataa kushiriki. Kwa njia hii, tunaamini kwamba wote watakubali kushiriki kwa faida yetu. Maana tunaamini kabisa kwamba asiyekubali kushiriki ni mwoga, hajiamini.
Tuliona hata mfano wa Uingereza juzi. Waziri Mkuu alidengua, alidengua, lakini mwisho ilibidi akubali na Waingereza walifaidi sana. Karibu nchi nzima waliangalia na kuweza kupima na kuamua. Kama hawa wakoloni waliotutesa waliweza kufanya hivyo, kwa nini sisi tuliomtoa mkoloni yuleyule hatuwezi kufanya vile? Nilisoma katika facebook (njia yetu sisi vijana kuwasiliana ndiyo maana tunawashukuru wagombea wenye kurasa zao humu … ingawa wanatakiwa kujibu maswali yetu pia!) jamaa mmoja akapinga kuwepo kwa mdahalo eti rais ni mtawala wetu hivyo hawezi kuongea na sisi watawaliwa, ni kinyume cha itifaki. Ha ha ha ha ha! Sasa kama mtawala haongei na sisi watawaliwa ataongea na nani? Wafadhili na mafedhuli? Ama kweli watu wengine wanachekesha.
Na hatuongelei upande wa urais tu. Siku hizi maredio ya FM yametapakaa kila mahali. Basi wagombea ubunge wa jimbo fulani na hata wagombea wa udiwani wafanye midahalo yao tuweze kupima na kuamua. Tunasema tena, mihotuba kibao, na ahadi dafrao hazitusaidii kuamua hata kidogo. Tunataka laivu, kila mmoja aonyeshe umahiri wa sera yake kwa kukabiliana na wenzake. Na mwenye sura badala ya sera, atokomee huko. Hatumtaki.
NO MDAHALO NO VOTE
Kwenye ngazi zote! Haya. Nije kwa wengine ambao pia wanataka tushike miguu ya watu (na ni wazi ukishika miguu ya mtu, lazima upige magoti mbele yake!) ni hao ambao wanadai wanataka kuendesha elimu ya uraia kwa wapiga kura. Nasikia mashirika mbalimbali, yakiwemo ya vijana wamepewa pesa kibao kujua kutuhubiria umuhimu wa kura zetu, tupige kura badala ya kuiuza, na maneno mengine yasiyo na mwisho. Kwani hatuyajui yote hayo? Ni sawa na kutuambia UKIMWI unaua na tubadili tabia. Tunajua na watu wanapewa nafasi ya kutafuna pesa kama wehu kwa kuja kututambia kwa kutuambia sifuri. Bora hata wangetuambia ufisadi unaua, mafisadi wabadili tabia, na kutupa nafasi ya kutafakari jinsi ya kuwakomesha mafisi wa ufisadi kabla hawajatutafuna wazimawazimu. Ndiyo, Makengeza. Sisi vijana tulifikiri elimu ya wapiga kura maana yake ni kutuwezesha sisi wapiga kura kukutana na kutoa mawazo yetu na kuandaa hoja za kumkabili kila mgombea si kukaa na kusikiliza hubiri zilezile kutokana na mamluki waliopewa pesa kwa ajili ya hubiri hizo.
Bora wangekuja kutuhubiri kwa kujitolea ha ha lakini lini hayo yatatokea? Hivi lini watu, wakiwemo wafadhili na mafedhuli, watajifunza kwamba hatusikilizi mihotuba ya walio nacho. Sisi tunatenda kutokana na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu sisi wenyewe. Kwa hiyo sisi vijana tunasema tunataka kushiriki kwa vitendo si masikio tu. Tunasema watu wasipoteze muda kutuhonga. Tumedhamiria na tutahongwa na mipango mizuri kwa vijana inayotekelezeka, si fedha, si ahadi ya fedha kama mabilioni ya huyu au yule.
Tutahongwa na sera si sura. Na kama vijana tutasimama imara kuhakikisha kwamba katika kila kituo cha kupiga kura, kila kata, na kila jimbo mafisadi hawatapewa nafasi ya kuharibu uchaguzi kwa kujaza kura feki, au kununua kura au mbinu zozote chafu. Na kama sote tumedhamiria hivyo, na tunatekeleza, tunao uhakika kwamba wenye nia mbaya ya uchaguzi, wanaoamini kwamba sisi tutakumbatia magoti ya watu ili mradi pesa tu, watakuja kujuta kwa nini walimwaga pesa zao zote bila mafanikio.
Ufisadi na wizi unawezekana kama tunauruhusu kwa kutofanya lolote. Narudia kusema Makengeza. Laiti vijana tungekuwa na chama chetu … lakini kwa kuwa hatuna, tutakuwa makini kusikiliza sera za kila chama, kila mgombea ili tuweze kumchagua yule ambaye kweli ataleta mabadiliko mazuri katika maisha yetu. Au vipi? Kijana asiyeinama bali anasimama imara. Jamani wasikia hayo. Vijana hawana utani mwaka huu. Asiyesikiliza asije akajuta baadaye.
No comments:
Post a Comment